Wastaafu: Mifumo TEHAMA imetuondolea 'panda, teremka' kufuatilia mafao

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:35 PM Jun 04 2024
Mwanaisha Mohammed Shosi (kushoto), Mwanachama wa PSSSF anayepokea pensheni ya kila mwezi, akiwa na mjukuu wake, wakati akielekezwa na Afisa wa PSSSF, Hamidu Nassoro namna ya kutumia huduma za PSSSF Kiganjani.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mwanaisha Mohammed Shosi (kushoto), Mwanachama wa PSSSF anayepokea pensheni ya kila mwezi, akiwa na mjukuu wake, wakati akielekezwa na Afisa wa PSSSF, Hamidu Nassoro namna ya kutumia huduma za PSSSF Kiganjani.

WASTAAFU wanaopokea pensheni kupitia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), wameeleza furaha yao ya kupata huduma za kujihakiki na malipo ya pensheni ya kila mwezi kupitia mifumo ya Kidijitali.

Wamesema hayo kwa nyakati tofauti walipofika kwenye banda la PSSSF katika Maonesho ya 11 ya Biashara na Utalii kwenye viwanja vya Usagara jijini Tanga.

“Mimi naishi Muheza, mfumo huu unanisaidia kuondoa adha ya kupanda mabasi kufuata huduma ofisi za PSSSF, sasa hivi ninajihakiki kupitia simu yangu ya kiganjani, pia tarehe ya malipo ya pensheni ikifika napokea ujumbe kwenye simu ukinionyesha kuwa pensheni yangu imelipwa.” amesema Khadija Almasi Fusi, mstaafu wa Chuo cha IDM, Mzumbe.

“Kilichonisisimua kufika kwenye banda lenu nikuja kutoa shukrani, ni ile hali ya kupokea pensheni yangu kwa wakati, ikifika tarehe 28 wakati mwingine 29, naona ujumbe wa simu kutoka PSSSF umeingia, mimi mbio benki kuchukua fedha zangu.” Amesema mstaafu mwingine Mwanaisha Mohammed Shosi.

Afisa Matekelezo PSSSF, Frederick Paschal (kushoto), akimuelekeza mwanachama wa PSSSF, jinsi ya kupakua App ya PSSSF Kiganjani.
Naye Francis Chimile Nkuba, yeye amesema, baada yaku kupakua App ya PSSSF Kiganjani amekuwa akipata huduma mbalimbali kiurasihi.

“Hivi sasa naweza kupata taarifa mbalimbali za Mfuko, lakini manufaa mengine ni kujihakiki mimi mwenyewe nikiwa nyumbani na maisha yakaendelea, inatusaidia tusiwe na safari za kwenda na kurudi kutafuta ofisi za PSSSF.” amebainisha Nkuba.

Aidha Afisa Mwandamizi wa PSSSF, Ally Amanzi, amesema sambamba na PSSSF Kiganjani, pia mwanachama anaweza kutumia Tovuti (Website) ya Mfuko, PSSSF Member portal kupata huduma kuhususiana na uanachama wake.
Mwanachama wa PSSSF, Francis Chimile Nkuba (kushoto), akielekezwa jinsi ya kupakua App ya PSSSF Kiganjani na Afisa wa Mfuko,Hamidu Nassoro.
“Kupitia PSSSF Member Portal, mwanachama anaweza kujisajili (Register Member) Kuhuwisha taarifa (Update Member) lakini pia kuwasilisha madai (Claim Submission).” alifafanua  Amanzi.