Utafiti wa kusambaza gesi Dar nzima kukamilika Juni

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 11:55 AM Apr 05 2024
Naibu Waziri Nishati, Judith Kapinga.
Picha:Mpigapicha Wetu
Naibu Waziri Nishati, Judith Kapinga.

WIZARA ya Nishati kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa kushirikiana na Kampuni ya TAQA Dalbit inafanya utafiti za mahitaji ya gesi asilia na njia za kusambazia katika Jiji la Dar es Salaam, ukitarajiwa kukamilika Juni 2024.

Naibu Waziri, Judith Kapinga aliyasema hayo bungeni jana alipojibu swali la Mbunge wa Kawe (CCM), Josephat Gwajima ambaye alihoji lini serikali itaweka mabomba ya gesi katika jiji hilo kila nyumba ili wananchi wapikie nishati safi na nafuu.

Akijibu swali hilo, Judith alisema hatua hiyo itawezesha kuwa na mpango madhubuti wa usambazaji gesi asilia utakaozingatia kero ya  mipango miji katika jiji hilo.

“Utafiti huu utaonesha namna bora ya kufikisha mabomba na kuainisha maeneo yanayofaa na yasiyofaa kupelekewa mabomba ambapo njia nyingine zitatumika kuhakikisha gesi inafika kwa wananchi,” alisema.

Naibu Waziri Judith alisema serikali kupitia TPDC inaendelea na utekelezaji miradi mbalimbali ya usambazaji gesi asilia jijini Dar es Salaam.

“Hadi sasa serikali imeshasambaza gesi asilia kwa njia ya mabomba katika nyumba 880 katika Jiji la Dar es Salaam kwenye maeneo ya Sinza (226), Mikocheni (155), Kurasini (344) na Mwenge Mlalakuwa na Chuo Kikuu - UDSM (155),”alisema.

Pia alisema serikali imejenga bomba la gesi lenye urefu wa kilomita 12.4 kutoka Mwenge hadi Mbezi Beach kupitia barabara ya Bagamoyo.

“Bomba hilo lina matoleo katika maeneo mbalimbali ili kuweza kuunganisha wateja wa majumbani. Kwa kuanza tayari viwanda viwili na hoteli sita  zimeshaunganishwa na bomba hilo katika eneo la Mbezi Beach na itaendelea kuunganisha wateja wa majumbani kwa maeneo yanayopitiwa na bomba hili,”alisema.

Mbunge wa Viti Maalum, Esther Matiko alisema maeneo ya vijijini wamehamasika kutumia nishati safi lakini gharama ya ujazaji gesi ni kubwa na kuhoji mkakati wa kuweka ruzuku ili waondokane na matumizi ya kuni na mkaa.

Naibu Waziri Judith, akijibu swali hilo, alisema serikali inatarajia kukamilisha hivi karibuni mkakati wa nishati safi ya kupikia ili kukabiliana na vikwazo vinavyosababisha wananchi wasitumie gesi kupikia.