Usajili laini simu wapaa Zanzibar

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:40 AM Apr 24 2024
Usajili wa laini za simu.
PICHA: MAKTABA
Usajili wa laini za simu.

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imesema kuwa mwelekeo wa usajili wa laini za simu za mkononi Zanzibar unaonyesha ongezeko la asilimia 12 katika upatikanaji wa huduma za simu za mkononi miongoni mwa wananchi.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma imeyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk. Jabiri Bakari, takwimu za hali ya mawasiliano kipindi cha Januari hadi Machi, mwaka huu, zinaonyesha usajili wa laini za simu Unguja na Pemba uliongezeka kwa wastani wa asilimia 37.21  kati ya 2022 na Machi 2024. 

“Serikali inatekeleza mradi mkubwa Zanzibar kuwezesha watumiaji kupata huduma bora zaidi za mawasiliano ya simu za mkononi, hasa zenye ubora kwenye maongezi na kasi ya matumizi ya data. Novemba 2022 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilizindua ujenzi wa minara ya mawasiliano ya simu 42 katika shehia (kata) 39 Unguja na Pemba,” amesema.

Amesema mradi huo ni sehemu ya mpango unaosimamiwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na kwamba kwa Tanzania Bara, serikali inajenga minara 758 mipya na kuboresha mingine zaidi ya 300 na kuiongezea nguvu. 

Dk. Bakari amesema takwimu za TCRA zinaonyesha kwamba kuenea kwa laini za simu miongoni mwa watu kwa Unguja na Pemba kumefikia asilimia 45 na kwamba kuenea huko kulikuwa asilimia 26.5 Septemba 2022, miezi miwili kabla ya mradi.

“Asilimia ya huduma kufika kwa watumiaji imeongezeka kwa kati ya pointi mbili na nne kipindi cha Januari hadi Machi kulinganisha na kipindi kilichotangulia kutegemea teknolojia inayotumika,” amesema.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, simu za uzao wa tatu zimeenea kwa asilimia 88 kutoka asilimia 86 kipindi kilichotangulia na kwamba uzao wanne (4G) umefika asilimia 80 kutoka 79 huku uzao wa tano (5G) umefika asilimia 13.  

“Takwimu zinaonesha kuwa laini 72,496,095 zilikuwa zimesajiliwa Tanzania nzima. Kati ya hizi, asilimia 1.3 ni za mashine zinazowasiliana zenyewe. Januari 2024 kulikuwa na laini za simu 70,035,043 za matumizi ya kawaida zilizosajiliwa.,” amesema.

Mkurugenzi mkuu huyo amesema takwimu za TCRA zinaonesha kwamba Dar es Salaam inaongoza kwa laini milioni 13.3, ikifuatiwa na Mwanza, yenye laini 4.8 na Arusha yenye milioni  4.5. Mbeya na Dodoma zinafuata, zikiwa na laini milioni 4.2 na milioni 3.7 mtawalia. 

Kuhusu matumizi ya intaneti yameongezeka, kwa idadi ya watumiaji na data. Watumiaji wameongezeka kutoka 36,687,794 Januari 2024 hadi 36,771,612 Machi  2024, na kwamba kumekuwa na ongezeko la asilimia 37 la watumiaji wa intaneti kati ya Machi 2020 na Machi 2024, 26,832,089 hadi  36,771,612. 

“Taarifa inaonesha zaidi ya asilimia 99 ya watumiaji intaneti wanapata huduma kupitia vifaa vya mkononi.  Matumizi ya data yaliongezeka kufikia MB 3,702 MB kwa mtumiaji Machi 2024kutoka MB 2,957 Desemba 2023.Takwimu zinaonesha kuwa kuenea  kwa simu zenye uwezo mkubwa, yaani simu janja hadi kufikia asilimia 32.59 ya watu Machi 2024  kutoka asilimia  32.13 Desemba 2023.

Aidha, amesema kuenea kwa simu za kawaida kumepungua kutoka asilimia 85.62 Desemba 2023 hadi asilimia 85.56 Machi 2024 hali inayoashiria ongezeko la matumizi ya simu janja miongoni mwa wananchi.