Umeme vitongojini wainua uchumi-RC Sendiga

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:21 PM Feb 07 2026
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, amesema utekelezaji wa mradi wa kusambaza umeme kwenye vitongoji ni chachu muhimu ya kuinua uchumi wa wananchi wanaoishi vijijini.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, amesema utekelezaji wa mradi wa kusambaza umeme kwenye vitongoji ni chachu muhimu ya kuinua uchumi wa wananchi wanaoishi vijijini.

Sendiga amebainisha hayo leo mkoani Manyara wakati wa kikao na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kilicholenga kumtambulisha mkandarasi mzawa aliyeshinda zabuni ya kutekeleza mradi wa kupeleka umeme katika vitongoji 267 vya mkoa huo, Kampuni ya SAGEM COM ENERGY.

Amesema mradi huo, unaogharimu zaidi ya Shilingi bilioni 45.8, unatarajiwa kutekelezwa ndani ya kipindi cha miaka mitatu na utanufaisha vitongoji vilivyopo katika Wilaya za Babati, Hanang, Mbulu, Kiteto na Simanjiro.

Akizungumza katika kikao hicho, Sendiga amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa fedha zilizowezesha utekelezaji wa mradi huo muhimu, akisema utachangia kwa kiasi kikubwa kuboresha maisha na kuinua uchumi wa wananchi, hususan waliopo vijijini.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wakandarasi kufanya kazi kwa bidii, weledi na uadilifu ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati uliopangwa. Vilevile, ametoa wito kwa viongozi wa Serikali na wananchi kushirikiana kikamilifu na mkandarasi wakati wa utekelezaji wa mradi huo.

“Nikiwa kama Mkuu wa Mkoa, natoa maelekezo kwa Wakuu wa Wilaya kuhakikisha wanashirikiana na kwenda kumtambulisha mkandarasi kwa wananchi. Pia nitoe rai kwa wananchi kuipokea miradi hii ya kijamii kwa moyo mmoja na kupunguza vikwazo, kwani inaleta faida kubwa kwa jamii,” amesisitiza Sendiga.

Awali, akizungumzia utekelezaji wa mradi huo, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Herini Mhina, amesema Mkoa wa Manyara una jumla ya vitongoji 1,946, ambapo vitongoji 1,113 tayari vimefikishiwa nishati ya umeme.

Mhandisi Mhina ameongeza kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 vitongoji vyote nchini vinakuwa vimefikishiwa umeme, na kwamba REA imejipanga kikamilifu kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ili kufikia lengo hilo la kitaifa.