CHAMA cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU), kimeipongeza serikali kwa kuwahamisha watumishi waliokuwa wanalipwa kwa mapato ya ndani ya Halmashauri (GF)na sasa kulipwa kupitia Mfuko Mkuu wa Serikali (HAZINA).
Katibu Mkuu wa TALGWU,Rashid Mtima, alitoa pongezi hizo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam.
Alisema ombi na kilio hicho cha kuhamishwa kwa watumishi hao kilikuwa cha muda mrefu na kuanza utekelezaji mwezi Julai 2024 na tayari wanachama wao 465 kati ya 645 wameanza kulipwa kupitia mfuko mkuu huo wa serikali.
Alisema hatua hiyo ni kubwa iliyochukuliwa na serikali kwasababu itaondoa kero za muda mrefu na kuongeza ari na morali ya kufanya kazi.
''Pamoja na pongezi hizi tunaiomba tena serikali kuangalia upya na kufanya mchakato ili wanachama wetu 180 waliosalia katika Majiji na Manispaa ambao bado wanalipwa kwa mapato ya ndani ya Halmashauri nao waanze kulipwa kupitia HAZINA,'' alisema na kuongeza;
''Kigezo kinachotumika kwamba halmashauri walizopo zina makusanyo makubwa ya fedha zinazotokana na mapato ya ndani na kwamba ziendelee kuwalipa mshahara wanachama hawa, tunaona ni wazo jema lakini bado siyo suluhisho la kutatua kero ambazo wamekuwa wakipata hapo awali,'' alisema.
Mtima aliiomba serikali kuwalipa watumishi wengine waliosalia kupitia mfumo huo wa HAZINA, huku Wakurugenzi wa halmashauri nao kuhakikisha wanawalipa watumishi mishahara kwa wakati kama ambavyo inafanya HAZINA.
Alisema Halmashauri hizo ambazo bado zinalipwa kwa kupitia mapato ya ndani ni Geita Mji, Ilala Jiji, Manispaa ya Kinondoni, Mbeya Jiji, Jiji la Mwanza, Temeke Manispaa, Dodoma Jiji na Manispaa ya Morogoro.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED