TAKUKURU yakamata mawakala mbinu chafu mitandao ya kibenki

By Christina Haule , Nipashe
Published at 09:39 AM Apr 24 2024
Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Morogoro, Christopher Mwakajinga.
PICHA: MOIGAPICHA WETU
Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Morogoro, Christopher Mwakajinga.

TAASISI ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkoa wa Morogoro imewafikisha mahakamani mawakala wa huduma za kifedha wawili kwa tuhuma za kufanya mbinu chafu na kuwaibia wateja wanapofanya miamala ya kupitia akaunti zao za kibenki.

Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Morogoro, Christopher Mwakajinga, amesema hayo wakati akitoa taarifa ya robo tatu ya mwaka 2023/24 na kubaini mbinu hizo chafu zinazotumiwa na mawakala hao baada ya kupata taarifa kutoka wa wasiri wao na kuanza kuzifanyia kazi.

Amewataja waliofikishwa katika mahakama ya Wilaya ya Morogoro kuwa ni Juma Msuya na Jamhuri Yohana ambao Machi 18 walifunguliwa kesi ya jinai namba 7110 ya mwaka 2024 na walikana shtaka hilo na wako nje kwa dhamana.

Mwakajina amefafanua kuwa mawakala hao wasio waadilifu wana tabia ya kupokea fedha kutoka kwa wateja wanaohitaji huduma ya kuweka fedha katika akaunti zao za benki, lakini fedha hizohaziingizwi katika akaunti walizopewa na wateja wao na badala yake wanatoa stakabadhi batili (fake) za kielektroniki ili kuwaaminisha  wamewekewa fedha.

Aidha, ameishauri jamii kujenga tabia ya kuhakikisha wanapokea taarifa kupitia simu zao zinazoonesha kuwa wameingiza fedha benki na kusoma akaunti zao ili kuepusha na kukomesha mbinu hizo chafu.

"Vilevile, ninawakumbusha wananchi wanapohitaji huduma ya kuwekewa fedha katika akaunti zao za kibenki kupitia mawakala, wajiridhishe kiasi uhakiki wa fedha zao kama zimeingia katika akaunti zao kupitia ujumbe mfupi kwenye simu zao kabla ya kuondoka kwa wakala," amesema Mwakajinga.

Pia, ametoa onyo kwa mawakala wote nchini kutojaribu kufanya udanganyifu wa kujipatia fedha kinyume na matakwa ya leseni zao walizopewa na mamlaka husika kufanya biashara hiyo.

Wakati huo huo, Mwakajinga amesema TAKUKURU imefuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayohusiana na afya na elimu yenye thamani ya Sh. bilioni 9.0 ambayo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na kabaini miradi sita yenye thamani ya Sh. bilioni 4.5, ikiwa na upungufu na kuchukuliwa hatua mbalimbali.

Ametaja miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa shule ya sekondari ya wasichana, Duthumi wilayani Morogoro wenye thamani ya Shilingi bilioni tatu na ufuatiliaji wa mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Dakawa, wilayani Mvomero wenye thamani ya Sh. milioni 400 miradi ambayo uchunguzi wake unaendelea.

Ameitaja miradi mingine kuwa ni ujenzi wa Shule ya Sekondari Madoto, Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa wenye thamani ya Sh. milioni 500, ujenzi wa jengo la mama na mtoto mjini Ifakara wenye thamani ya Sh. milioni 500 na ujenzi wa matundu ya vyoo na sehemu ya kunawia mikono kwenye Shule ya Msingi Lilela wilayani Gairo, wenye thamani ya Sh. milioni 46.3 na ushauri mbalimbali umetolewa katika kuhakikisha ujenzi unakwenda kama ulivyopangwa 

Aidha, Mwakajinga ameitaja mikakati ya TAKUKURU kwa kipindi cha Aprili hadi Juni 2024 kuwa ni kutoa elimu ya uzuiaji vitendo vya rushwa kwa wanafunzi, wananchi na watumishi wa umma na kuendeleza programu ya TAKUKURU rafiki kwa kata ambazo hazijafikiwa na kutoa mrejesho wa kata walizopitia.