Taasisi za dini zatajwa utakatishaji fedha na ufadhili wa ugaidi

By Beatrice Shayo , Nipashe
Published at 10:03 AM Mar 27 2024
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamadi Masauni.
PICHA: FULL SHANGWE
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamadi Masauni.

TANZANIA imetajwa haina mifumo mizuri ya usimamizi na ufuatiliaji mienendo wa jumuiya za kiraia, zikiwamo taasisi na madhehebu ya dini, hali inayotengeneza hatari ya kutumika katika utakatishaji fedha haramu au kufadhili ugaidi.

TANZANIA imetajwa haina mifumo mizuri ya usimamizi na ufuatiliaji mienendo wa jumuiya za kiraia, zikiwamo taasisi na madhehebu ya dini, hali inayotengeneza hatari ya kutumika katika utakatishaji fedha haramu au kufadhili ugaidi.

Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamadi Masauni, wakati akizindua kampeni za usajili wa jumuiya nchini.

Amesema baadhi ya jumuiya za kiraia zimeripotiwa kujihusisha au kutumika katika kufanikisha kutendeka kwa makosa ya jinai na vitendo vingine vyenye madhara kwa jamii.

Ametaja miongoni mwa makosa hayo ni utakatishaji fedha haramu, ugaidi na ufadhili wa shughuli za kigaidi, usafirishaji haramu wa binadamu, biashara haramu ya silaha na kuwapo jumuiya za kidini zinazotoa mafundisho potofu na hatarishi kwa usalama wa raia (afya ya mwili na akili).

“Madhara yatokanayo na kuchelewa kutoa ufumbuzi wa changamoto nilizozitaja hapo juu pamoja na udhaifu wa mifumo ya fedha katika taasisi hizo, umepelekea Taasisi ya Kimataifa ya Financial Action Task Force (FATF) ambayo ilianzishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kutoa ripoti ambayo inaonesha kuwa nchi yetu haina mifumo mizuri ya usimamizi na ufuatiliaji mienendo wa jumuiya za kiraia, zikiwamo taasisi na madhehebu ya dini.

“Hali hiyo inatengeneza mazingira rafiki ya taasisi hizo kutumika au kuwa katika hatari ya kutumika katika utakatishaji fedha haramu au kufadhili masuala ya ugaidi," amesema.

Waziri huyo aliitaja ni hali iliyosababisha Tanzania kuwekwa katika kundi la nchi zinazohitaji ufuatiliaji wa karibu (Enhanced Monitoring).

"Hivyo, ni lazima tushirikiane kwa karibu katika kuondoa hali hii kwenye nchi yetu,” alisema Masauni na kuongeza kuwa vyombo vya kimataifa na wadau mbalimbali wa kimataifa wamekuwa wanapewa tahadhari kuhusu udhaifu wa kusimamia jumuiya hizo ambao unaweza kutumika katika masuala utakatishaji fedha haramu na ufadhili wa ugaidi.

Waziri Masauni amesema hali hiyo inaweza kuleta madhara ya kuharibu taswira nzuri ya kidiplomasia iliyomo katika nchi.

“Ninaendelea kusisitiza umuhimu wenu katika kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambayo kupitia Ofisi ya Msajili wa Jumuiya inatekeleza Mpango Kazi wa FATF utakaowezesha serikali kuondolewa kwenye kundi hili, pia kufanikisha jukumu la kudumisha amani na utulivu katika maeneo yetu,” amesema.

Waziri Masauni amesema licha ya faida alizozitaja zitokanazo na jumuiya zilizosajiliwa, hivi karibuni kumeibuka wimbi la kutumia jumuiya za kiraia katika kufanya vitendo vinavyohatarisha amani na usalama wa nchi.

Waziri amesema kuna baadhi ya jumuiya zinatumika katika kusaidia makundi yenye dhima ya kigaidi, kusambaza propaganda za uchochezi, kuwasilisha ajenda za kigeni au wafadhili wa nje ambao ajenda zao zinaweza kuhatarisha maslahi ya taifa ikiwamo mmonyoko wa maadili.

Amesema ni muhimu kwa jumuiya za kiraia kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni za maadili, uwazi na uwajibikaji ili kuhakikisha wanachangia katika maendeleo ya jamii bila kuhatarisha ulinzi na usalama wa nchi au kusababisha mmonyoko wa maadili.

Ameeleza kuwa serikali ina jukumu la kusimamia na kudhibiti shughuli za jumuiya za kiraia ili kuhakikisha zinafanya kazi kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi. 

Waziri huyo pia amesema kumebainika changamoto ya uanzishwaji holela na utitiri wa nyumba za ibada katika maeneo mbalimbali nchini.

“Baadhi ya jumuiya za dini, hususan makanisa na misikiti, zimebainika kujengwa katikati ya makazi ya watu, kuna mrundikano wa taasisi nyingi kwenye eneo dogo na baadhi ya taasisi kutumia sauti za juu na hivyo kusababisha adha na usumbufu katika jamii,” amesema.

Kwa upande mwwingine, waziri huyo amesema jumuiya za kiraia zina mchango mkubwa katika kuleta mabadiliko chanya katika jamii na kuchangia katika maendeleo endelevu ya jamii na taifa kwa ujumla katika kuchochea ubunifu na ukuaji wa uchumi, utoaji huduma za kijamii, zikiwamo za elimu na afya.

Amesema jumuiya za kiraia zilizosajiliwa zina uwezo wa kushirikiana na serikali, mashirika ya kimataifa na wadau wengine katika miradi na shughuli za maendeleo.

Ameeleza kuwa usajili unaweza kuwa muhimu katika kuanzisha ushirikiano na kupata rasilimali na msaada kutoka kwa wadau hao na kudumuisha uwazi na uwajibikaji.

"Ni lazima kisheria kuandaa na kuwasilisha taarifa za fedha za mapato na matumizi ya jumuiya ambazo hutakiwa kuwasilishwa na kupitishwa na wanachama kupitia mikutano mikuu ya jumuiya zao kabla ya kuwasilishwa katika Ofisi ya Msajili wa Jumuiya,”ameagiza.

Amesema wizara yake imekuwa inashirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kufanya kazi kwa karibu na ofisi za makatibu tawala wa mikoa na ofisi za wakuu wa wilaya katika ufuatiliaji mienendo na usimamizi wa jumuiya kupitia kamati za usalama zilizoko katika ngazi za mikoa na wilaya.

Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Sospeter Mtwale, amesema watashirikiana na wizara na kuchukua hatua dhidi ya jumuiya ambazo zinakwenda kinyume cha taratibu za nchi.