Simulizi walioambulia 'kiduchu' bomoabomoa Bonde la Msimbazi

By Beatrice Shayo , Nipashe
Published at 06:03 PM Mar 27 2024
Sehemu ya Bonde la Msimbazi jijini Dar es Salaam.
PICHA: MAKTABA
Sehemu ya Bonde la Msimbazi jijini Dar es Salaam.

NYUMBA 2,155 zilizomo katika Bonde la Msimbazi, jijini Dar es Salaam zinatarajiwa kubomolewa kuanzia Aprili 12, mwaka huu baada ya wamiliki wake kulipwa fidia ya Sh. bilioni 52.61 kupisha mradi wa kuendeleza bonde hilo.

Hata hivyo, taarifa za bomoabomoa hiyo zimeibua kilio kwa baadhi ya wananchi, wakiwamo wapangaji wa nyumba zilizoko eneo hilo, wakidai wenye nyumba wamechukua kodi licha ya kuwa na taarifa kwamba nyumba zao zitabomolewa.

Mjumbe wa Shina Mtaa wa Madaba, Jamila Juma, akizungumza na Nipashe, amesema ni miongoni mwa waliogomea fidia ya awali ambayo aliandikiwa kulipwa Sh. milioni  saba, jambo ambalo hakuridhishwa nalo.

Amesema kwa sasa amelipwa fidia ya Sh. milioni 12 na baada ya muda aliongezwa Sh. milioni nne ambazo alijulishwa wameongezwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema fedha aliyolipwa imeishia kununua kiwanja na hakuwa anajua kama nyumba yake itabomolewa Aprili 12, mwaka huu, jambo ambalo limemshangaza.

Jamila amesema awali walijulishwa kuwa katika mradi huo, fidia ya nyumba ni Sh. milioni 200, lakini walicholipwa ni tofauti na uhalisia wa maisha.

"Mimi nilikuwa nina matumaini ya Sh. milioni 200, basi kama ningekosa hiyo, basi hata wangesema kila mmoja wanamlipa Sh. milioni 50 ambao tuna nyumba ili ununue kiwanja na kujenga lakini matokeo yake tumeambulia fedha kiduchu, yupo mtu aliyelipwa Sh. 27,000, huu mradi umekuja na maumivu," amesema.

Agustina Francis (54), amesema bado hajalipwa fidia yake kwa kuwa awali walimwambia fidia yake ni Sh. milioni saba, akawagomea na alivyofanyiwa tathmini nyingine, anasuburia kulipwa Sh. milioni 38.

Mpangaji katika eneo hilo, Veronica William, amesema hana taarifa ya kubomolewa nyumba, mwenye nyumba amekuwa anapokea kodi huku akiwajulisha nyumba hiyo haiwezi kubomolewa.

"Mimi nimesikia baba mwenye nyumba kalipwa fidia, lakini hajatuambia wapangaji wake kama tunatakiwa kuondoka na amekuwa hata mkataba hatupatii na kodi tumemlipa. Kwahiyo, zinakuja kubomolewa Aprili 12, hata hatujui.

"Jamani, ninakushukuru kwa kuniambia, maana ningedhalilika wangekuja kutubomolea na mali zetu zingepotea daah! Ngoja nianze kutafuta nyumba nyingine, jamani! Mbaya ni huyu baba mwenye nyumba, anachukua kodi na kukaa kimya," amelalama.

BIL. 52/- ZA FIDIA 

Mratibu wa miradi ya ushirikiano na Benki ya Dunia (WB) na Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA), Humphrey Kanyenye, aliwaambia waandishi wa habari jijini juzi kuwa watu 2,155 kati ya 2,329 waliomo kwenye daftari la kwanza wamekwishapokea malipo yao ya Sh. bilioni 52.61 kupisha mradi wa kuendeleza bonde hilo.

"Hii 'yard' ya mabasi ya mwendokasi itahamishiwa Ubungo Maziwa, ni sehemu ya kazi ya mkandarasi, lengo la mradi huu ni kujenga mto kwa ajili ya kuzuia mafuriko yanayotokea katika eneo hilo na tutajenga City Park (Maegesho ya Jiji) ambayo itaongoza kwa ukubwa," ametamba.

Mratibu huyo alisema mradi huo una mambo matatu; kujenga daraja, ujenzi wa mto na kuhamisha kituo cha mabasi ya mwendokasi na kujenga Maegesho ya Jiji, ukigharimu Dola za Marekani milioni 260.

Kanyenye alisema ofisi ya uratibu wa mradi kwa kushirikiana na ofisi za wakurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam na Manispaa ya Kinondoni wanatarajia kuanza ubomoaji nyumba zilizofidiwa kuanzia Aprili 12, mwaka huu, yaani siku 17 zijazo.

Amesema awamu hiyo ya utekelezaji zoezi hilo itawahusu wale ambao wamefikisha wiki sita zilizotolewa baada ya kupokea malipo ya fidia hadi kufikia Februari 29, mwaka huu.

Amesema daftari la pili la waathirika 446 ambao hawakufikiwa katika uthamini wa awali kwa sababu ya kugomea fidia hiyo na kudai ni ndogo kwa sasa wameshakubali na kutia saini.

Amesema daftari lilitarajiwa kuwasilishwa kwa Mthamini Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kutiwa saini jana Machi 26, mwaka huu tayari kulipwa fidia.

"Wananchi ambao wana maswali au wanahitaji maelezo zaidi kuhusu ubomoaji  wanaweza kuwasiliana na ofisi ya uratibu wa mradi wa Bonde la Msimbazi kupitia namba ya WhatsApp 0738353854 kwa kutuma ujumbe au kupiga namba 0738353855 kupata majibu ya maswali yote kuhusiana na mradi huo," amesema.