KATIKA kuwalinda wasichana wenye umri wa kuanzia miaka 9 hadi 14 dhidi ugonjwa wa saratani ya mlango wa shingo ya kizazi, Mkoa wa Shinyanga unakusudia kuanza kampeni ya utoaji wa chanjo ya HPV, huku Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Joseph Mkude akisema mkoa umejipanga kuwafikia watoto wa kike 198,865.
Taarifa kutoka mkoani humo inaonyesha kampeni hiyo, inatarajia kuanzia Aprili 22 hadi 28, hata hivyo; utoaji wa chanjo hiyo utakuwa endelevu hadi Desemba mwaka huu.
Akizungumza leo April 19, 2024; mkoani hapa, DC Mkude, ambaye amemuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga katika kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi, ametaka elimu iltolewe ili walengwa wote wafikiwe.
"Utoaji wa chanjo hii, unaongeza kinga kwa wasichana wenye umri wa miaka 9 hadi 14 dhidi ya ugonjwa saratani ya mlango wa shingo ya kizazi, hivyo natoa wito kwa wazazi, kuwaruhusu mabinti zao wapate chanjo hii, ili kulinda afya za watoto wao," amesema Mkude.
Aidha, amewaagiza viongozi wa Serikali wakiwamo Watendaji wa Kata na Vijiji, kuwabaini wasichana ambao hawapo mashuleni ili waweze kupata chanjo hiyo.
Amewaagiza pia wataalamu wa afya watakatoe elimu juu ya chanjo hiyo katika nyumba za ibada.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk. Yudas Ndungile, amesema utoaji wa chanjo hiyo ya HPV ulianza Mwaka 2014; kwa kutolewa dozi mbili, hata hivyo baada ya mabadiliko, itatolewa kwa dozi Moja.
"Tafiti za kisayansi zimethibitisha kuwa dozi moja ya chanjo ya HPV inatosha kutoa kinga kamili dhidi ya maambukizi ya saratani ya mlango wa shingo ya kizazi," amesema Ndungile.
Naye Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Shinyanga, Timothy Sosoma, amesema chanjo hiyo, itatolewa Shuleni kwa shule zote za msingi na sekondari 887, pamoja na kwenye vituo vya afya 241.
Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Paul Julius, ameupongeza Mkoa wa Shinyanga, kutokana na maandalizi mazuri ya utoaji chanjo hiyo, na kwamba ametembelea baadhi ya maeneo ambapo vitendea kazi vya utoaji chanjo, vimeshafika maeneo husika.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED