SHERIA MPYA MAFAO: Mlolongo ahueni kwa mchangiaji

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 07:46 AM Aug 30 2024
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete
Pichagapicha Wetu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete

BUNGE limepitisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria za Hifadhi ya Jamii wa Mwaka 2024 wenye mlolongo wa mambo kadhaa yenye ahueni kwa mchangiaji.

Katika muswada huo, waajiri wamepunguziwa adhabu ya kuchelewa kuwasilisha michango na kutoa rukhsa kwa mfanyakazi aliyeajiriwa na mwajiri zaidi ya mmoja kuchangiwa na wote kwa ridhaa yake. 

Vilevile, mwanachama ambaye hajafikia umri wa kustaafu, ameruhusiwa kutumia sehemu ya mafao yake kama dhamana kwa mkopo wa nyumba huku watu waliojiajiri wenyewe katika sekta binafsi wakiruhusiwa kujiunga na kunufaika na mafao ya hifadhi ya jamii katika mpango wa uchangiaji kwa mujibu wa sheria. 

Muswada huo pia umeruhusu michango iliyowekwa na mwanachama baada ya umri wa kustaafu hadi kufikia miaka 70 kuzingatiwa katika ukokotoaji malipo ya mafao ya pensheni. 

Akiwasilisha muswada huo bungeni jana, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, alisema marekebisho hayo yanagusa sheria tatu ambazo ni Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii, Sura ya 50; Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma, Sura ya 371; na Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi, Sura ya 263. 

Waziri huyo alisema kimeongezwa kifungu cha 11A kinacholenga kuongeza wigo wa hifadhi ya jamii kwa watu waliojiajiri. 

Pia alisema muswada huo umemruhusu mwajiri kuchangia kwa kiasi kikubwa au kiasi chote na Kifungu cha 12(5) kimependekezwa kurekebishwa kuainisha namna ya uchangiaji kwa wanachama waliojiajiri. 

"Kifungu cha 12A kimeongezwa ili kuruhusu mfanyakazi aliyeajiriwa na mwajiri zaidi ya mmoja kuchangiwa na waajiri wote kwa ridhaa yake. Lengo la marekebisho haya ni kumpa mwanachama uhuru wa kuchangiwa na zaidi ya mwajiri mmoja," alisema. 

PUNGUZO LA ADHABU

Ridhiwani alisema kifungu cha 14(3) kimerekebishwa ili kupunguza adhabu ya tozo kutoka asilimia tano (5) hadi asilimia mbili na nusu (2.5) inayotozwa na mfuko kwa mwajiri kwa kuchelewa kuwasilisha michango ya mfanyakazi na lengo ni kuainisha kiasi stahiki cha faini na kupunguza gharama za uendeshaji kwa waajiri na kuweka tozo rafiki na zinazolipika. 

Ridhiwani alisema wameongeza makosa mapya kwa mwajiri anayekataa kujiandikisha na mtu yeyote anayemzuia mkaguzi wakati wa kutekeleza majukumu yake, kumwezesha Mkurugenzi wa Mashtaka au ofisa wa mfuko aliyeteuliwa na Mkurugenzi wa Mashtaka kufungua kesi yoyote ya jinai chini ya sheria. 

Waziri huyo alisema muswada huo umependekeza kumwezesha Mkurugenzi Mkuu kuteua jopo la madaktari ili kuthibitisha iwapo mwanachama amepata ulemavu wa kudumu na lengo la ni kuhakikisha mafao yanatolewa kwa mnufaika anayestahili. 

Pia alisema muswada umeongeza kiwango kinacholipwa kwa wategemezi pale ambapo mwanachama atakuwa amefariki dunia kutoka miezi 33 hadi 36. 

Alisema muswada umeweka masharti ya lazima kwamba waajiriwa wa kampuni ambayo serikali inamiliki angalau asilimia 30 ya hisa, ni lazima wasajiliwe kwenye Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).

 Alisema pia muswada huo unaboresha masharti yanayohusiana na kumbukumbu za michango ya mwajiriwa pindi itakapohitajika ili kumwezesha mwanachama kupata historia ya uchangiaji wake kwenye mfuko.

 â€œKifungu cha 24 kimefutwa ili kuondokana na dhana iliyojengwa katika kifungu hicho inayoruhusu mwanachama kutoa kiasi cha mchango wake katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii na kuondolewa uanachama, inakinzana na Kanuni za Hifadhi ya Jamii kutokana na dhana ya kifungu hicho kutumiwa kwenye Mfuko wa Akiba na si katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii," alisema.

 WALIO GEREZANI

Ridhiwani alisema masharti yamewekwa mnufaika wa mafao ambaye kwa kipindi husika anatumikia kifungo, anaweza kuridhia kwa maandishi kwamba mafao yake au sehemu yoyote ya mafao yake ilipwe kwa mnufaika atakayetajwa.

 "Lengo la marekebisho haya ni kuimarisha ushiriki wa mtu anayetumikia kifungo katika utoaji mafao yake kwa mnufaika," alisema.

 Waziri huyo alisema kifungu cha 48(6) kinapendekezwa kurekebishwa ili kumwezesha mwajiriwa ambaye amepata ulemavu wa kudumu kuendelea kupokea pensheni hata baada ya kurejea kazini au kupokea mafao ya uzeeni.