RAIS Samia Suluhu Hassan amesema serikali ina mpango wa kuajiri wahudumu wa afya 137,000 na tayari mchakato wa kuwapata umekamilika ngazi ya halmashauri.
Amesema mafunzo ya kundi la kwanza yameanza mwezi huu (Julai) katika vyuo vya afya nchini.
Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akifunga kumbukizi ya tatu ya Hayati Benjamin Mkapa iliyoandaliwa na Taasisi ya Benjamin Mkapa na kuhudhuriwa pia na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Kumbukizi hizo zimehudhuriwa pia na viongozi wa serikali, wastaafu na wake wa viongozi wakuu wastaafu wakiongozwa na mama Anna Mkapa.
Rais Samia alitaja hatua nyingine za kutengeneza ajira kwa watumishi kada ya afya kuwa ni ziara zinazofanyika nchi mbalimbali kuzungumza nazo kama zina uhitaji huo wawachukue.
“Nilikuwa ninazungumza na Ofisa Mtendaji Mkuu wa taasisi hii kwamba, kundi la kwanza la wauguzi 200 kwa kushirikiana pia na taasisi hii tayari wameshakwenda na wameanza kazi na tunatengeneza kundi la pili,” alisema.
Rais Samia aliitaka Ofisi ya Waziri Mkuu iimarishe timu ya kuratibu rasilimali katika sekta ya afya ili ifanye kazi zake.
Kadhalika aliitaka Wizara ya Afya kukamilisha utafiti wa kitaifa kubainisha hali halisi ya wataalam wa afya walioko soko la ajira na kufahamu nguvu kazi iliyoko nje katika vituo vya tiba.
Pia, aliitaka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kutengeneza mkakati wa diplomasia ya afya na kusaidia upatikanaji wa nafasi za mafunzo ya juu ya utaalam kwa watumishi wa sekta hiyo.
Alisema amezungumza na Mtendaji wa Global Education Link (GEL) ambaye amemweleza kwamba, wanazungumza na vyuo duniani ili kupeleka wanafunzi fani za afya kwa fedha ambazo zingelipwa ndani ya nchi.
Alisema urithi alioacha Benjamin Mkapa unafanya aendelee kuishi hata baada ya kifo chake.
Alisema miaka minne tangu atangulie mbele ya haki, Mzee Mkapa anakumbukwa kama baba wa taasisi, mifumo na wa mageuzi, na alitumia muda mwingi wa hotuba zake kuelezea mambo hayo matatu katika sekta zote.
“Ndio maana wadau wengi wa maendeleo wameelekeza nguvu zaidi kudhibiti maradhi ya kuambukiza na kidogo kwenye miundombinu ya afya. Ni ukweli kwamba mafanikio yake yanategemea watumishi wa afya wa kutosha na wenye weledi,” alisema.
Rais Samia alisema kujenga kituo cha afya inaweza kukamilika ndani ya mwaka mmoja ikiwa fedha zipo wakati inahitajika miaka sita kumwandaa daktari mmoja na walau miaka mitatu kumwandaa muuguzi huku dakati bingwa huchukua miaka tisa hadi 12.
Alisema kupoteza mtumishi mmoja sekta ya afya ni hasara kubwa kwa taifa, kulinganisha na uwekezaji mkubwa wanaofanya.
“Ninapozunguka mikoani changamoto namba moja ninayokutana nayo ni ya watumishi katika sekta ya afya na elimu. Kwa nini sekta hizi, idadi ya watu inakua kwa haraka, tunazaliana mno na mahitaji ni makubwa mno. “Ajira zinaendana na ukuaji uchumi tukipata nafasi kidogo uchumi ukikua kidogo hapo hapo tunasema sekta ya afya na elimu,” alisema.
Aidha, alisema changamoto ya upungufu wa watumishi imesababisha serikali kutanua wigo ufadhili wa masomo mikopo ya elimu ya juu.
Rais Samia alisema takwimu zilizotolewa katika mkutano huo zinaonesha kuna upungufu wa asilimia 60 na kueleza kwamba, kuna jitihada za kuajiri watumishi wengi kwa miaka mitano.
Alisema taasisi za kidini zinajitahidi kuingia sekta ya afya ingawa wafanyakazi wa hospitali hizo mategemeo ni serikalini.
“Wengi wamejikita katika utoaji huduma na katika miradi ya afya kwa jamii, kutengeneza nguvu kazi ni mzigo wa serikali peke yake, zikijipanua tunakuwa na mzigo mkubwa wa wafanyakazi,” alisema.
Aliihakikishia BWF na taasisi zingine kwamba, kadri serikali inavyotoa ajira wataalam wa afya wa mkataba walioko kazini wataendelea kuhuhishwa katika ajira za serikali.
Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ambaye ni Msarifu wa Taasisi ya BMF, alisema kuwapo kwa taasisi hiyo kumechangia nguvu kazi ya rasilimali watu
Alisema kwa upande wa Zanzibar wanaendelea kujenga miundombinu ya afya na kuendelea kutoa ajira na kuboresha mazingira ya kazi kwa kujenga nyumba za watumishi wa afya.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, alisema serikali imeongeza posho za madaktari anapoitwa nje ya saa za kazi, posho za sare za wauguzi na ile ya kuchunguza maiti kuanzia mwaka huu wa fedha.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini BMF, Dk. Adeline Kimambo, alisema Mpango Mkakati wa miaka sita (2024/30) wa Taasisi hiyo uliozinduliwa juzi, pamoja na mambo mengine umelenga kuimarisha afya na ustawi wa jamii nchini na nje ya nchi ambao pia, utaongeza watanzania wengi kuwa na bima ya afya.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo, Dk. Ellen Mkondya- Senkoro, alisema Hayati Mkapa amewaachia urithi mwingi ambao unatakiwa kuendelezwa kizazi hadi kizazi, akiishukuru familia yake, kupitia mke wake, Anna Mkapa, kuwaamini na kumega sehemu ya urithi wa familia kwa ajili ya watanzania.
Akitoa salamu za familia ya Hayati Mkapa, William Erio, alimshukuru Rais Samia kwa kuendelea kumtunza mama Mkapa na wadau waliofanikisha kumbukizi hiyo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED