Samia ampa simba jina la Lissu, azindua utalii wa kasa

By Waandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:47 AM Aug 25 2024
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan akiangalia uzuri wa pango pamoja na Kasa ambao wamekuwa kivutio cha watalii, baada ya kuzindua Utalii wa Kasa katika Pango la Salaam, Kizimkazi Dimbani, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar jana.
PICHA: IKULU
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan akiangalia uzuri wa pango pamoja na Kasa ambao wamekuwa kivutio cha watalii, baada ya kuzindua Utalii wa Kasa katika Pango la Salaam, Kizimkazi Dimbani, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar jana.

RAIS Samia Suluhu Hassan ameelekeza simba dume katika Tamasha la Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja, visiwani Zanzibar, aitwe Tundu Lissu.

Kwa mujibu wa kiongozi aliyekuwa akitoa maelezo kwa Rais Samia katika tamasha hilo jana, simba huyo ambaye yumo ndani ya banda alimohifadhiwa akiwa anazunguka huku na huko, alisema moja ya tabia za simba huyo anapoona watu huwa hivyo, lakini hana tatizo. 

Baada ya maelezo hayo, Rais Samia aliuliza jina la simba huyo na alipoelezwa kwamba hajapatiwa jina, ndipo aliposema aitwe Tundu Lissu. 

Rais Samia wakati akifanya ufunguzi wa bwawa la kisasa la kuhifadhia kasa ikiwa ni miongoni mwa matukio katika Tamasha la Kizimkazi kwa mwaka huu, aliwataka wananchi kulitumia kama fursa za kujijenga kiuchumi na kulinda utamaduni wa nchi.  

Alisema kuwapo tamasha hilo kunachangia kwa kiasi kikubwa shughuli za uwekezaji pamoja na kupanua mji huo, hivyo ni vyema wananchi kuchangamkia fursa zilizoko. 

Alisema kuna fursa nyingi ambazo zinapatikana Kizimkazi hasa zinazohusu sekta ya utalii wa bahari pamoja na mapango ya kale. 

Rais Samia alipongeza jitihada kubwa zilizofanywa kwa sekta ya utalii Zanzibar na kueleza kuwa kuna haja ya kutunza mazingira kwa kuhifadhi viumbe vya baharini kama kasa. 

Alisema kasa licha kuwa kivutio cha utalii, watapata sehemu ya kuhifadhiwa na baadaye kurejeshwa baharini. 

"Niwapongeze kwa jitihada kubwa mlizofanya kwa kubuni jambo hili ambalo kwanza, limetunza mazingira na uhifadhi bora," alisema. 

Rais Samia alisema kivutio hicho cha utalii kitaingizwa katika mtandao wa vivutio vya utalii Tanzania ili kuwavutia wageni wengi zaidi.  

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Ayoub Mohmed, alisema mkoa huo una wastani wa vivutio 17, zikiwamo fukwe za bahari, misitu na majengo ya asili. 

Alisema wageni wengi wanaokwenda kutalii huko huangalia samaki aina ya pomboo (dolphine) na msikiti wa kale pamoja na kasa. 

Alisema kuwapo tamasha hilo la Kizimkazi kumeongeza kivutio cha utalii, pia kutaongeza idadi ya watalii wanaotembelea mkoa huo. 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk. Ashatu Kijazi, alisema eneo hilo ni muhimu na linatengeneza ajira pamoja na uchumi wa taifa na kuwa mfano wa kutunza mazingira.

*Imeandaliwa na Romana Mallya na Rahma Suleiman