Samia aeleza umuhimu AU kuzingatia mageuzi kikatiba

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 07:15 AM Aug 28 2024
RAIS Samia Suluhu Hassan.
Picha: Mpigapicha Wetu
RAIS Samia Suluhu Hassan.

RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema nchi za Afrika zina wajibu wa kuhakikisha Umoja wa Afrika (AU), unaendelea kushikamana kwa kuzingatia malengo makuu na muhimu yaliyowekwa ikiwamo kuzingatia mageuzi ya kikatiba.

Pia, nchi hizo zitambue zinawajibu wa kuimarisha uwajibikaji na kuweka silaha chini na kuupa nafasi umoja huo kutimiza malengo iliyojiwekea ikiwamo ajenda ya maendeleo.

Aliyasema hayo jana akiwa Nairobi, nchini Kenya katika hafla ya uzinduzi wa kampeni ya Raila Odinga, Waziri Mkuu mstaafu wa Kenya, anayewania nafasi ya Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU).

“Pamoja na hatua zilizofikiwa na umoja huu, kuna haja ya kuyafikia malengo makuu kwa kuhakikisha, sauti zetu, sauti za Waafrika zinasikika kwenye mijadala ya kidunia, hasa katika mabadiliko ya tabianchi kuingia kwenye nishati safi.

Kufikia maendeleo ya Akili Mnemba (AI) duniani. Hii ina maana kwamba Serikali ya Tanzania inamthibitisha Raila Odinga, kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU). Tanzania inamfahamu Odinga kwamba ni Mwafrika kiongozi anayeamini katika ushirikiano kivitendo,” alisema Rais Samia.

Alisema, Raila mwenye taaluma ya uhandisi anafahamu AU inahitaji zaidi miundombinu ili kuondokana na pengo lilimo kwenye sekta hiyo ili kufikia Afrika imara na yenye uwezo.

“Odinga anaweza kusimama imara katika kuhakikisha kipaumbele cha maendeleo kwa Afrika kinazingatiwa. Tanzania inawahakikishia kwamba inaungana na Wakenya, kumuunga mkono Odinga kuwania nafasi hiyo…baba anatosha, achaguliwe,” alisema Samia.

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni alisema kwamba tatizo kubwau liliopo miongoni mwa nchi za kiafrika ni umaskini, unaohitaji kupatiwa ufumbuzi kwa kuhakikisha kuna huduma muhimu bora za kijamii.

“Tunahitaji madaktari wa kiuchumi kwenye jamii na ukiangalia jamii zetu Afrika utajiuliza nini tatizo, makabila, dini zipo. Tukaja tukabaini ugonjwa mkubwa ni ustawi duni kwenye jamii, umaskini.

“Watu wanahitaji chakula, malazi, elimu na kwa namna gani watavipata? Unahitajika ustawi wa kijamii. Watu kama wanazalisha mali bila hesabu, wanashindwa kufanya uchambuzi watashindwa kuondokana na umaskini,” alisema Museveni.

Alisema katika yote kikubwa kinachohitajika ni uzalendo kutoka kwa wananchi wa bara hilo, kwa kununua bidhaa zinazolishwa nchini mwao ili kuinua kiwango cha soko na uchumi wa ndani.

Hafla hiyo imehudhuriwa pia na Rais Museveni; Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini, Salva Kiir Mayardit; Waziri Mkuu wa Burundi, Gervais Ndirakobuca na viongozi wengine.