Ripoti ya CAG yadai Ulaji bado upo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:50 AM Apr 16 2024
Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, charles kichere.
PICHA: MAKTABA
Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, charles kichere.

RIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, imeonesha kuwa ununuzi na usimamizi wa mikataba katika mamlaka 35 za serikali za mitaa wa jumla ya Sh. bilioni 4.22 ulifanyika bila kuitisha nukuu za ushindanishi wa bei.

Aidha, mamlaka 16 za serikali za mitaa, zenye ununuzi wa jumla ya Sh. bilioni 4.87 ziliamua kutumia njia ya mzabuni mmoja au wachache badala ya njia ya ushindanishi bila sababu za kuridhisha. 

Hayo yamo kwenye ripoti kuu ya mwaka wa ukaguzi wa Serikali za Mitaa kwa mwaka wa fedha 2022/23, ambayo pia ilibaini mamlaka 13 za serikali za mitaa zilinunua bidhaa zenye thamani ya Sh. bilioni 1.45 ambazo hazikupokewa licha ya malipo kufanyika.

HASARA KITUO CHA MABASI

“Kuhusu usimamizi wa mikataba, ilibainika kuwa mkandarasi na mkandarasi mshauri waliohusika na usimamizi wa ujenzi wa Kituo Kikuu cha Mabasi cha Halmashauri ya Jiji Dar es Salaam kilichopo Mbezi Luis, walikuwa hawajalipwa ankara zao za jumla ya Sh. bilioni 8.92, hivyo kusababisha madai ya riba ya Sh. bilioni 2.23,” amesema.

MFUMO WA TAUSI

CAG amebaini pamoja na kuanzishwa kwa Mfumo wa Ukusanyaji Mapato Serikalini (TAUSI) na maelekezo mahususi kwa mamlaka za serikali za mitaa kusajili mashine za kukusanyia mapato (POS), kufanya usuluhishi kwa wadaiwa kwenye mfumo wa awali wa LGRCIS, na kutumia moduli zote ndani ya TAUSI kwa ukamilifu, bado kuna Sh. bilioni 45 ambazo ni madai ya mapato yasiyokusanywa kwenye mfumo. 

UKUSANYAJI MAPATO

Aidha, amebaini jumla ya Sh. bilioni 61 hazikukusanywa na mamlaka 130 za serikali za mitaa, kutoka vyanzo mbalimbali kama vile kodi ya maduka, vibanda vya soko, kodi ya nyumba, mauzo ya viwanja, ukusanyaji wa taka, leseni za biashara, leseni za vileo, maeneo ya wazi yaliyokodishwa, ada za maegesho, na vyanzo vingine vya mapato, ikiashiria kukosa ufanisi katika ukusanyaji wa mapato. 

“Katika kupitia taarifa za mifumo ya LGRCIS na TAUSI, nilibaini kuwa jumla ya Sh. bilioni 6.2 ambazo ni mapato yaliyokusanywa kupitia mashine za POS katika mamlaka za serikali za mitaa 96, hazikuwa zimewasilishwa benki za mamlaka za serikali za mitaa husika.”

“Usimamizi wa matumizi tathmini yangu ya usimamizi wa akaunti ya amana unaofanywa na mamlaka za serikali za mitaa iliibua kasoro kadhaa zenye jumla ya Sh. bilioni 10.71 katika akaunti za amana zinazomilikiwa na mamlaka za serikali za mitaa,” imebainisha ripoti hiyo. 

MADAI WAZABUNI

Ripoti hiyo imebainisha kuwa katika mamlaka za serikali za mitaa 37 kuongezeka kwa madai ya wazabuni na wafanyakazi kutoka Sh. bilioni 64.87 kwa mwaka wa fedha 2021/22 hadi Sh. bilioni 87.32 kwa mwaka wa fedha 2022/23, ikiashiria ongezeko kubwa la Sh. bilioni 22.45, sawa na asilimia 35. 

Kuhusu usimamizi wa rasilimali watu katika mamlaka 54 za serikali za mitaa, alibaini madai ya watumishi yenye jumla ya Sh. bilioni 36.47 ambayo hayajalipwa kwa zaidi ya miezi 12. 

Madai hayo yanajumuisha malimbikizo ya mishahara ya wafanyakazi, stahiki za wastaafu, na stahiki zingine kama vile posho za kisheria kwa wakuu wa idara na vitengo. 

Ulinganifu wa taarifa za mishahara kutoka kwenye Mfumo wa Taarifa za Usimamizi wa Rasilimali Watu (HCMIS) na kanzidata ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), ulibaini utofauti mkubwa.

“Mathalani, utofauti wa tarehe za kuzaliwa ulibainika kwa watumishi 77,286 katika takwimu za kanzidata zote mbili, na kusababisha mkanganyiko kuhusiana na tarehe sahihi za kuzaliwa kwa watumishi wa umma. Nilibaini kuwa hapakuwa na takwimu zozote za watumishi 86 katika kanzidata ya NIDA,” amesema.

Aidha, amesema tathmini yake ya mifumo ya uhasibu wa Mfumo wa Ulipaji Serikalini (MUSE) ambao umechangia katika dosari zilizobainika wakati wa ukaguzi wa miamala iliyofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe na kubaini malipo ya jumla ya Sh. bilioni 1.23, yalifanywa kupitia akaunti ya mishahara kwa shughuli ambazo hazikufanyika. 

MIRADI YA MAENDELEO

Mamlaka za serikali za mitaa 20 zenye miradi yenye thamani ya Sh. bilioni 8.04 ambayo imekamilika, lakini haitumiki, na kutofikiwa malengo yaliyokusudiwa. 

Vilevile, CAG amebaini dosari mbalimbali katika miradi yenye thamani ya Sh. bilioni 13.81 iliyotekelezwa na mamlaka 14 za serikali za mitaa. 

ELIMU BILA MALIPO

Ufanisi wa uendeshaji sekta ya elimu katika mwaka wa fedha 2022/23, ulikuwa na upungufu wa ruzuku ya elimu bila malipo iliyotolewa kwa mamlaka za serikali za mitaa 15 kwa ajili ya shule za msingi na sekondari, ikiwa jumla ya Sh. bilioni 1.25 kati ya Sh. bilioni 11.83 zilizokuwa zimepangwa katika bajeti ya kipindi hicho. 

CAG amesema TAMISEMI ilitoa jumla ya Sh. bilioni 10.6 kwa Taasisi ya Elimu Tanzania kwa ajili ya ununuzi wa vitabu vya shule za msingi, ambayo iliingia mkataba na kampuni nne za uchapaji na usambazaji wa vitabu milioni 2.51, lakini hakukuwa na ushahidi wa kuthibitisha usambazaji wa vitabu hivyo. 

MIRADI BILA EIA

Mbali na hayo, CAG amebaini miradi yenye thamani ya Sh. bilioni 635.12 ilianza bila kuwa na cheti cha tathmini ya athari kwa mazingira (EIA) na kijamii, wakati ununuzi wenye thamani ya Sh. bilioni 7.12 kwa taasisi 15 ulifanyika bila kuidhinishwa na bodi za zabuni.

Pia amebaini upungufu kwenye michakato ya utoaji zabuni, ambapo taasisi 16 zilifanya ununuzi wenye thamani ya Sh. bilioni 149.56 bila kutumia mfumo wa kielektroniki.

Kadhalika, taasisi sita zilifanya ununuzi wenye thamani ya Sh. bilioni 77.67 bila kutumia njia za ushindani wa bei. Ununuzi wa bidhaa zenye thamani ya Sh. bilioni 2.16 ulifanyika bila kutumia mikataba na mikataba yenye thamani ya Sh. bilioni 4.78 haikupekuliwa na wanasheria.

Amebaini upungufu katika kutimiza majukumu ya kimkataba ambapo taasisi 11 zilichelewa kulipa madai ya Sh. bilioni 38.73 na kutolipa madai ya Sh. bilioni 19.37 ndani ya muda uliokubaliwa.

Wizara ya Ujenzi haijalipa riba ya Sh. bilioni 17.48 iliyotokana na uamuzi wa usuluhishi uliofikiwa tangu mwaka 2014 pamoja na riba ya Sh. bilioni 34.82 iliyotozwa kwa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa kuchelewa kulipa makandarasi.

Pia mikataba 46 ya ujenzi ilikosa dhamana za utendaji kazi zenye thamani ya Sh. bilioni 383.76.

CAG pia amebaini Tume ya Madini na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) hazikudai dhamana ya utendaji kazi na malipo ya awali yenye thamani ya jumla Sh. milioni 675.90 kwenye mikataba iliyositishwa.