Rais Samia kushiriki ibada miaka 40 ya kifo cha Sokoine

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 07:03 PM Mar 28 2024
Msemaji wa familia ya Hayati Sokoine Lembris Kipuyo gumza na wanahabari leo kuhusu ibada hiyo itafanyika Aprili 12, 2024, saa 3:00 asubuhi.
Picha: Paul Mabeja.
Msemaji wa familia ya Hayati Sokoine Lembris Kipuyo gumza na wanahabari leo kuhusu ibada hiyo itafanyika Aprili 12, 2024, saa 3:00 asubuhi.

RAIS Samia Suluhu Hassan, atarajiwa kuwaongoza viongozi mbalimbali pamoja na baadhi ya Watanzania kwenye ibada maalum ya kumbukizi ya miaka 40 ya Hayati Edward Moringe Sokoine, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, itakayofanyika Aprili 12, 2024, katika Kijiji cha Enguik, Monduli Juu mkoani Arusha.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa Msemaji wa familia ya Hayati Sokoine Lembris Kipuyo, amesema ibada hiyo itafanyika Aprili 12, 2024, saa 3:00 asubuhi, ambapo imeandaliwa na familia ikishirikiana na Taasisi ya Hayati Edward Moringe Sokoine.

Amesema ibada hiyo ya kumbukumbu ya Hayati Sokoine itawashirikisha viongozi mbalimbali wa serikali wakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Akizungumzia lengo la kuanzishwa kwa Taasisi ya Hayati Edward Moringe Sokoine, amesema ni kuenzi mema aliyoyafanya kwani aliacha alama kubwa ambayo taifa linamkumbuka hadi leo. 

Pia, amesema Taasisi hiyo imejikita katika masuala ya elimu, kilimo, hifadhi ya mazingira, vyanzo vya maji pamoja na afya.

Kipuyo, amesema Hayati Sokoine alifanya mambo makubwa sana katika Taifa la Tanzania ambayo hadi leo yameacha alama kubwa hivyo kupitia siku hiyo Watanzania watapata fursa ya kuelewa kile alichokifanya wakati wa uhai wake.

'Hayati Sokoine alikuwa mzalendo wa kweli, alipenda taifa lake na wananchi wake, alihakikisha kwamba rasilimali za nchi zinatumika na Watanzania wote, aliwatumikia wananchi bila kubagua na alikuwa na hofu ya Mungu katika kufanya kazi zake"amesema

Aidha, amesema katika mambo ambayo hayatasahahulika ni pamoja na jitihada zake kwenye kilimo na mifugo, ambapo yeye ndiye alikuwa chachu ya kuanzishwa kwa Chuo kikuu cha Kilimo Sokoine, ambacho kilianzishwa kwa lengo la kuzalisha wataalam wa kilimo ili kuiwezesha nchi kuwa na uhakika wa chakula.

Hayati Sokoine alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika vipindi viwili wakati wa uongozi wa Awamu ya Kwanza. Alizaliwa Agosti 01, 1934, kijijini Enguik, Monduli Juu wilayani Monduli, mkoani Arusha.