Rais Samia aahidi neema JWTZ

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:20 AM Aug 24 2024
Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Dk. Samia Suluhu akiimba pamoja na vikundi mbalimbali vya askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wakati wakitoka kwenye zoezi la Medani.
Picha: Ikulu
Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Dk. Samia Suluhu akiimba pamoja na vikundi mbalimbali vya askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wakati wakitoka kwenye zoezi la Medani.

RAIS na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Samia Suluhu Hassan amesema atasimamia shabaha ya kuwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) madhubuti na lenye maofisa na askari wenye weledi, ari na zana bora.

Aliyasema hayo jana wakati akifunga zoezi la Medani katika kuadhimisha Miaka 60 ya JWTZ katika eneo la Pongwe Msungura, lililoko Msata.  

Rais Samia alisisitiza kuwa jeshi imara zaidi litatokana na dhamira ya kweli, moyo wa kujituma na uchumi imara zaidi.   

Vilevile, Amiri Jeshi Mkuu aliitaka JWTZ kuendelea kulinda misingi ya kuanzishwa kwa jeshi hilo na kuendelea kudumisha nidhamu, utii, uaminifu na uhodari uliopo katika jeshi hilo. 

Rais Samia pia alisisitiza JWTZ kuendelea kuwa Jeshi la Wananchi la ukombozi la mfano kwa Afrika na dunia kwa namna linavyoonesha uhodari, weledi na nidhamu ya kijeshi. 

Mkuu wa Nchi pia alishukuru Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa kushirikiana na JWTZ katika zoezi la Medani lililojumuisha mazoezi ya baharini na nchi kavu.  

Pia alipongeza ujio wa meli kubwa ya hospitali ya kijeshi iliyotoa huduma ya vipimo na matibabu kwa wananchi takribani 8,000. 

Kupitia mazoezi hayo, JWTZ imebadilishana uzoefu kuhusu mbinu mbalimbali za kupambana na ugaidi, uvuvi haramu, uharamia, usafirishaji haramu wa watu na dawa za kulevya.