Mtahabwa: Serikali yafikiria kuifunga shule muda wowote

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 08:42 AM Apr 24 2024
Kamishna wa Elimu katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Lyabwene Mtahabwa.
PICHA: MAKTABA
Kamishna wa Elimu katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Lyabwene Mtahabwa.

SERIKALI inafikiria kufunga shule muda wowote kuanzia sasa kutokana na athari za mvua inayoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini.

Kamishna wa Elimu katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Lyabwene Mtahabwa, amesema kuwa serikali inafanya tathmini kwa kuhusisha athari ya mvua katika mikoa yote nchini kabla ya kuchukua uamuzi huo. 

Akizungumza na mwandishi wa habari hii kwa njia ya simu kuhusu athari ya mvua inayoendelea sasa na hatua zilizochukuliwa kwa watoto shuleni, Dk. Mtahabwa, amesema: “Tulia, nimeandika barua. Hilo  jambo tunalishughulikia ili tufanye tathmini mikoa yote na athari zake.

“Ikiwezekana tufunge shule kwa siku kadhaa ili watoto wawe salama. Tunalifanyia kazi, kiongozi wangu tuko makini sana. Ninashukuru sana kwa kuliona hilo, ubarikiwe,” amesema.

Kuhusu lini taarifa ya kufungwa shule itatolewa, Dk. Mtahabwa amesema wakati wowote kuanzia sasa zitatolewa na hicho ndicho kipaumbele chao kwa sasa.  

Wakati hatua hii ikichukuliwa, Aprili 12, mwaka huu, basi la wanafunzi katika Shule ya Mchepuo wa Kiingereza ya Ghati Memorial School ya jijini Arusha, lilitumbukia kwenye korongo lililoko eneo la Engosheratoni, Kata ya Sononi, na kusababisha vifo vya watoto saba.

Awali, Kaimu Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi, Butusyo Mwambelo, akizungumza na Nipashe kuhusu athari ya mvua kwa upande wa miundombinu, amesema kwa ujumla hali ni mbaya na imesababisha baadhi ya barabara kufungwa kwa muda.

 “Mfano, barabara ya Jangwani tumeifunga tangu jana (juzi) baada ya mvua kunyesha na maji kujaa. Magari yote yanaishia Magomeni na yanayotokea mjini yanaishia Fire.

“Barabara ya Nyerere, kutokana na ujenzi kuna baadhi ya maeneo yana mashimo mengi. Pia pale Vingunguti kuna ujenzi unaoendelea, shimo limejaa maji. Tunatahadharisha  wananchi na wenye magari madogo  na vyombo vingine vya moto wanapotumia barabara hii, wawe makini,” amesema.

Kadhalika amesema eneo la Kigamboni kutokea Tungi Msikitini kuelekea katika mzunguko wa kwa Msomari kuna shimo limejaa maji.

Barabara zingine zilizoripotiwa kufungwa kutokana na maji kujaa ni Mkwajuni, Africana na ile ya kutokea Kibada kuelekea Kisarawe 2 daraja limekata mawasiliano baada ya kuvunjika.

Hadi mwishoni mwa wiki mvua hii ya masika iliathiri jumla ya wananchi 273,159 kwa wakazi wa mikoa ya Pwani, Morogoro na Mbeya na kusababisha kukosa makazi.

Amesema tayari Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalum ya Dar es Salaam (ZCO) na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, wamekwenda kufanya ukaguzi kwa sababu maji yamejaa na barabara hazipitiki.

Mwambelo amesema wametoa tahadhari pia kwa wanafunzi kuwa makini hasa wanaporuhusiwa kwenda shuleni.

“Magari yanayochukua wanafunzi mengi ni madogo na yanapita barabara ambazo si za lami na mitaro mingi imeziba. Kama wanaona ni hatari ni bora shuleni wasiende kuchukua wanafunzi au wasiende shuleni kabisa ili tusisababishe maafa mengine.

“Mpaka sasa upande wa usalama barabara hatujapata maafa yoyote. Kwa upande mwingine nimewasiliana na Kamishna wa Elimu kuangalia kwa kipindi hiki kila mtu aangalie eneo lake kama kuna mvua nyingi watoto wasiende shule.

“Yaani wakafunga shule angalau siku mbili au tatu. Amepokea ombi letu na ametuambia atawasiliana na TAMISEMI (Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa) ameliona wazo hili ni zuri na ameahidi kulifanyia kazi,” amesema.

Mwambelo amesema wameona shule zikifungwa kwa kuwa kuna zingine zimeshafungwa kutokana na kuathiriwa na mafuriko, watoto hawatakuwa nyuma kielimu.

DART

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma cha Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), kuanzia jana, barabara ya Jangwani ilifungwa kutokana na mafuriko, hivyo mabasi ya njia ya Gerezani, Kivukoni yataishia Magomeni Mapipa.

Taarifa hiyo imesema huduma ya usafiri wa DART inaendelea kutolewa kwa njia ya Morocco kwenda Kimara na maeneo ya katikati ya jiji kwa njia ya Muhimbili na Gerezani.

Pia imesema huduma za mabasi ya mfumo wa DART zinaendelea kama kawaida kwa njia ya Kimara hadi Mbezi, Kimara hadi Kibaha na Kimara hadi Mlongazila.