KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Godfrey Mnzava, ameagiza kuanzia sasa Mfumo mpya wa Ununuzi wa Umma wa Kielektroniki (NeST) usiwe kificho, badala yake watu wapewe elimu ya namna unavyochakata taarifa.
NeST ilianzishwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), kwa ajili ya kusaidia kudhibiti rushwa, mchakato wa zabuni kuchelewa na kuongeza uwazi wa zabuni.
Akiwa katika Kijiji cha Kimashuku, Kata ya Mnadani, Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, leo Aprili 3, 2024, Mwenge ulikokwenda kuweka jiwe la msingi la Zahanati ya Kijiji hicho, Mnzava amesema:
"DC (Mkuu wa Wilaya), DED (Mkurugenzi Mtendaji), mambo machache tu ya kusisitiza, ambayo pia nimekueleza pale ndani.
"Kama ambavyo mnafahamu serikali yetu imeelekeza juu ya udhibiti wa manunuzi ya umma.
"Na katika maelekezo hayo tumeendelea kusisitiziwa kuhakikisha manunuzi yote yanapitia katika MFUMO na mfumo huu unaitwa NEST.
...Iwe ni fedha kutoka vyanzo vya mapato, wahisani, hakikisha fedha hizo zinapitia kwenye mfumo.
Zaidi amesisitiza, "Wananchi waombe zabuni kupitia mfumo na mfumo wenyewe utachakata na kueleza nani na nani ana sifa za kupata hiyo tenda.
"Kama Halmashauri tuwajengee uwezo watumishi na watendaji wetu, Zahanati na vutuo vyetu vya kutoa huduma, shule na taasisi za umma jinsi mfumo unavyofanya kazi."
Mwenge wa Uhuru umekagua,kuweka jiwe la msingi na kuzindua miradi yenye thamani ya Sh. 995,725.202.
Miradi iliyozinduliwa ni uhifadhi wa chanzo cha maji Njoro (Kata ya Mnadani), ujenzi wa tangi la maji Rundugai (Kata ya Masama Rundugai) na ujenzi wa Zahanati ya Kimashuku (Kata ya Mnadani).
Mwingine ni ujenzi wa barabara ya lami Bomamg'ombe, km 0.3 kwa kiwango cha lami, mradi wa vijana wa ungenezaji wa samani kwa kutumia vioo na aluminium (Kata ya Bomamg'ombe) na ujenzi wa shule mpya ya sekondari (Saashisha Sec-Kata ya Muungano).
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED