Mganga akwepa kifungo cha miaka miwili jela kisa rushwa

By Halima Ikunji , Nipashe
Published at 08:45 AM Apr 18 2024
Daktari akwepa jela kisa rushwa.
PICHA: MAKTABA
Daktari akwepa jela kisa rushwa.

MAHAKAMA ya Hakimu Mfawidhi Wilaya ya Nzega mkoani Tabora, imemhukumu Mtumishi wa Idara ya Afya ambaye ni mganga wa hospitali ya mji mdogo wa Nzega, Daudi Ashim Msokwa (29) kutumikia adhabu ya kifungo cha miaka miwili jela baada ya kukiri kosa la kuomba rushwa kutoka kwa mgonjwa aliyekuwa akitibiwa.

Awali, Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Wilaya ya Nzega, Mazengo Joseph, akishirikiana na Shabani Mntambo, wadai mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Nzega, Saturin Mushi, kuwa mshitakiwa April 16, mwaka huu katika hospitali ya mji mdogo wa Nzega aliomba rushwa ya Sh. 150,000 kwa Christina Aroiz (39), mkazi wa Nzega ambaye alikuwa amempeleka mgonjwa Gaudensia Eugene (25) aliyekuwa amelazwa na kufanyiwa upasuaji.

Joseph alidai mtuhumiwa aliomba kiasi hicho cha fedha kutoka kwa ndugu wa mgonjwa ili aweze kumruhusu kuondoka hospitalini hapo baada ya mtuhumiwa kumfanyia oparesheni.

Aidha, Mazengo alidai mahakamani hapo kuwa mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 15(1) (a), (2), (3)(a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa sura ya 329 marejeo ya 2002 inayozuia kutenda makosa kama hayo.

Mshitakiwa alikiri kutenda kosa hilo. Hata hivyo, Mwendesha Mashtaka Joseph alidai upande wa Jamhuri hawaoni sababu ya kupeleka mashahidi mahakamani kwa kuwa mshitakiwa amekiri mwenyewe.

Baada ya maelezo hayo Hakimu Mushi alisema: “Kwa kuwa mshitakiwa amekiri mwenyewe shitaka lake mbele ya mahakama inamtia hatiani mshitakiwa na kumpa adhabu ya miaka miwili jela au kulipa faini ya Sh. 500,000 ili iwe fundisho kwa wengine.

Mshitakiwa alilipa kiasi hicho cha fedha na kuwa huru.