Mkataba kampuni ununuzi mwani kuvunjwa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:29 AM May 01 2024
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Burian (wapili kushoto) akiwa na wakulima wa mwani.
Picha: Mtandaoni
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Burian (wapili kushoto) akiwa na wakulima wa mwani.

SERIKALI mkoani hapa imesema itavunja mkataba na kampuni zinazokiuka makubaliano ya kuwakopesha wakulima wa mwani pembejeo za kilimo.

Msimamo huo ulitangazwa juzi na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Burian, wakati akizungumza na wafanyabiashara na kampuni zinazonunua zao hilo.

Ni  baada ya kuwatembelea wakulima wa zao hilo katika wilaya za Muheza, Tanga, Mkinga na Pangani walioingia makubaliano hayo na kampuni hizo ya kukopeshwa pembejeo hizo. 

Balozi Buriani, alisema haiwezekani wanunuzi wa zao hilo wakaingia mkataba na wakulima na kushindwa kutoa pembejeo hizo na kusababisha wahangaike.

“ Ninyi wanunuzi kama hii kazi imewashinda tutavunja mikataba na turudi kwa wakulima wetu na tuwaambie Benki ya Kilimo watoe mikopo yenye riba chini ya asilimia nne mpaka tatu,” alisema na kuongeza kuwa: “Tunajua kabisa wakikopeshwa wanaweza kununua kamba, taitai na troliki na kufanya kilimo chenye tija na faida.”

Awali, Ofisa Mfawidhi wa Idara ya Ukuzaji wa Viumbe Maji, Mkoa wa Tanga, Omari Mohamed, alisema serikali imekuwa ikisaidia na kusimamia na kuna mikopo ambayo haina riba.
 
Mohamed, alisema Wizara ya Mifugo na Uvuvi inashirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo kuwakopesha wakulima hao pembejeo na boti za uvuvi.

Alisema awamu ya kwanza ilikwisha kufanyika na wapo kwenye awamu ya pili. “Awamu ya pili tutatoa pembejeo kwa wakulima wa mwani nchi nzima.” 

Hata hivyo, alisema kwa sasa serikali inaangalia sehemu zenye mapungufu ili iweze kusaidia.