TAKUKURU yawabana wakopaji, warejesha mamilioni

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:08 AM May 01 2024
Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Tanga,Victot Swella.
Picha: Mpigapicha Wetu
Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Tanga,Victot Swella.

ZAIDI ya Sh. milioni 439.27 za mikopo inayotokana na ruzuku ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika Halmashauri ya Jiji la Tanga, imerejeshwa serikalini baada ya wanufaika waliogoma kurejesha kubanwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Fedha hizo ni kati ya Sh. bilioni 2,152.229 zilizokuwa hazijarejeshwa kwa wakati kutoka kwa wanufaika wa mikopo hiyo.

 Kwa mujibu wa Kamanda wa TAKUKURU mkoani hapa, Victot Swella, miongoni mwa mambo waliyobaini katika ufuatiliaji wa fedha hizo ni kukiukwa kwa masharti ya kurejeshwa mikopo hiyo.

 Ufuatiliaji huo ni utendaji kazi wa TAKUKURU wa kipindi cha kati ya Januari hadi Machi mwaka huu.

Alisema baada ya kulibaini hilo, taasisi hiyo iliwakutanisha wadau na kuweka mapendekezo ya kurejesha fedha hizo na hadi kufikia Februari mwaka huu, Sh. milioni 439,279,300.00 zilirejeshwa katika halmashauri hiyo.

 Hadi sasa Sh. 1,712,950,600 hazijarejeshwa na kwamba jitihada za ufuatiliaji zinaendelea.
 
Vilevile katika kipindi hicho, walifuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo 46 yenye thamani ya Sh. 8,041,998,680.00 katika sekta za elimu, barabara, maji na afya.
 
 Katika ufuatiliaji huo walibaini miradi 32 yenye thamani ya Sh. 4,866,068,966.00 ina mapungufu na kushauri kurekebisha kupitia vikao na wadau husika.