Leo Mei 21,2024 katika ukumbi wa Bali International Convention Center nchini Indonesia, Tanzania imeungana na nchi nyingine duniani katika Kongamano la 10 la Maji Duniani (10th World Water Forum) ambalo limepitisha Azimio la Mawaziri (Ministerial Declaration on Water for Shared Prosperity).
Azimio hilo ambalo msingi wake ni mikataba na maazimio mbalimbali ya Umoja wa Mataifa kuhusu maji kama vile Maji ni Haki ya Binadamu limeibua changamoto za maji duniani kama vile mabadiliko ya tabianchi pamoja na kasi ndogo ya dunia kulifikia lengo namba 6 la Malengo ya Endelevu ya Umoja wa Mataifa linalohusu maji.
Aidha, Azimio hilo linatoa hamasa ya kutatua changamoto hizo kwa kuwa na ubunifu na uendelevu wa upatikanaji wa fedha za maji (Innovative and sustainable financing) pamoja na uongozi na utashi wa kisiasa.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso anamuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan katika kongamano hilo lililohusisha wakuu wa nchi mbalimbali pamoja na mawaziri na wawakilishi wa mataifa mbalimbali.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED