Mgosi aitaka heshima ya Simba Queens, bado 7 tu

By Saada Akida ,, Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 06:51 AM May 01 2024
Kocha Msaidizi wa Simba Queens, Mussa Hassan ‘Mgosi',.
Picha: Simba SC
Kocha Msaidizi wa Simba Queens, Mussa Hassan ‘Mgosi',.

LICHA ya kubakiza pointi saba tu kabla ya kutangazwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara msimu wa 2023/24, Kocha Msaidizi wa Simba Queens, Mussa Hassan ‘Mgosi', amesema bado wana safari ngumu kuhakikisha wanaendelea kurejesha heshima ya klabu hiyo.

Simba Queens juzi waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya wapinzani wao wakuu, JKT Queens, katika mchezo wa ligi hiyo uliochezwa Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam.

Yalikuwa ni mabao ya straika hatari wa timu hiyo, Aisha Mnuka na beki wa kati wa Kimataifa wa Kenya, Ruth Ingosi, yaliyoifanya timu hiyo, si tu kupata ushindi huo, lakini kufikisha jumla ya pointi 37, ambazo zinaifanya kuhitaji ushindi wa michezo miwili na sare moja katika michezo mitano iliyobaki ili kuweza kutwaa ubingwa huo.

Takwimu zinaonyesha kuwa iwapo Simba Queens itapata pointi saba, itafikisha jumla ya pointi 46 ambazo hazitafikiwa na timu yoyote ile kwenye Ligi Kuu ya Wanawake inayozishirikisha timu 10.

Wakati timu zote zikiwa zimecheza mechi 13 na kubakisha mechi tano tu, Mabingwa Watetezi, JKT Queens baada ya kufungwa juzi wamebaki na pointi 28, ambazo kama ikishinda mechi tano zilizobaki itafikisha pointi 43, ambazo zitakuwa zimeshapitwa na Simba Queens, iwapo itashinda mechi mbili au tatu zijazo.

Akizungumza na Nipashe baada ya mchezo huo juzi, Mgosi alisema pamoja na kuifunga JKT Queens, bado ligi inaendelea hivyo wanatakiwa kupambana kila mechi kusaka pointi tatu muhimu kufikia malengo yao yanayotarajiwa hususan kutwaa ubingwa wa ligi hiyo.

Mgosi alisema mipango yao ni kuona wanafanikiwa kwenye malengo yao ikiwamo kurejesha heshima ya klabu hiyo hali ambayo inahitaji kushinda michezo iliyopo mbele yao.

Aidha, aliwapongeza wachezaji wake kwa kufuata maelekezo na kuweza kupata ushindi na kurejesha heshima ya klabu hiyo kwa kumfunga JKT Queens.

“JKT Queens ni timu kubwa hapa nchini, kupata heshima Simba lazima uifunge timu kubwa kama JKT Queens, tumefanikiwa kumfunga mkubwa mwenzetu, lakini bado hatujachukua ubingwa ambayo ni malengo yetu.

"Kufikia malengo hayo ni lazima tupambane kushinda michezo iliyopo mbele yetu yote, kuifunga timu kubwa haina maana kuwa tupo bora zaidi kwa sababu tunaenda kukutana na timu zingine ambazo zimejipanga vizuri na unapokosea unaadhibiwa,” alisema Mgosi.

Kocha wa JKT Queens, Ester Chabruma, alisema walijiandaa vizuri kwa mchezo huo na wamepoteza kwa makosa  waliyoyafanya uwanjani ambayo yaliwafaidisha Simba kwa kupata ushindi.

“Kuhusu kutetea ubingwa wetu kwa sasa tuna mlima mrefu kutokana na Simba Queens kutuzidi alama tisa, lakini bado tutaendelea kupambana kwa sababu ligi bado haijaisha," alisema Chabruma. 

Bingwa wa ligi hiyo, huiwakilisha nchi kwenye michuano ya CECAFA, ambayo pia hutumika na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), kumpata mwakilishi wa Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kwa timu inayotwaa ubingwa huo.

Simba Queens na JKT Queens zimeiwakilisha Ukanda wa CECAFA mwaka juzi na uliopita zilipotwaa ubingwa na Afrika Mashariki na Kati.