Mbunge ahoji raia wa kigeni kuwa meneja rasilimaliwatu wa Dangote

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 11:14 AM Nov 07 2024
MBUNGE wa Mtwara Mjini (CCM), Hassan Mtenga.
Picha: Mtandao
MBUNGE wa Mtwara Mjini (CCM), Hassan Mtenga.

MBUNGE wa Mtwara Mjini (CCM), Hassan Mtenga ameihoji serikali sababu ya raia wa Nigeria kuajiriwa kama Meneja Rasilimaliwatu wa Kiwanda cha Saruji Dangote mkoani Mtwara ilhali sheria inakataza.

Akiuliza swali bungeni jana, mbunge huyo alisema suala hilo ni la muda mrefu lina miaka mitatu na meneja huyo yupo na kuhoji ni sababu gani zinakwamisha kuondolewa kwake.

"Ninaomba twende kwenye kiwanda cha Dangote akaone uhalisia wa jambo hili tunalozungumza,” alisema.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi, alisema malalamiko yanayotolewa na mbunge yalishafika wizarani na kufanyiwa kazi.

“Kwa kuzingatia Sheria ya Kuratibu Ajira za Wageni, Sura 436 na Sheria ya Uwekezaji Tanzania, Na. 10 ya mwaka 2022, ofisi ilifanya ukaguzi maalum katika kiwanda hicho tarehe 23 na 24, Septemba, 2024 ili kujiridhisha na ukweli wa malalamiko haya na utekelezaji wa Sheria za Kazi kwa ujumla. Serikali ilithibitisha malalamiko hayo,” alisema.

Hata hivyo, alisema kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za serikali, wanaendelea kushughulikia suala hilo na litakapokamilika, hatua stahiki zitachukuliwa.

Alisema serikali haina kigugumizi kuchukua hatua na kwamba wamechelewa kutokana na kubaini kuna uvunjifu wa sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai.

“Tayari polisi inaendelea kufanya uchunguzi wa makosa yaliyotendeka, sambamba na Idara ya Uhamiaji na Ofisi ya Waziri Mkuu tunaendelea kuyashughulikia, kama tungechukua hatua haraka kuna makosa ya jinai ambayo tungewanyima haki waliotendewa,” alisema.