Makinda : Hayati Sokoine hakuwa mnafiki alitufundisha uaminifu na ukweli

By Beatrice Shayo , Nipashe
Published at 08:41 PM Sep 25 2024
Makinda : Hayati Sokoine hakuwa mnafiki alitufundisha uaminifu na ukweli
Picha:Mpigapicha Wetu
Makinda : Hayati Sokoine hakuwa mnafiki alitufundisha uaminifu na ukweli

ALIYEKUWA Spika wa Bunge, Anne Makinda, amesema enzi za uhai wa Waziri Mkuu Mstaafu, Hayati Edward Sokoine, aliwafundisha ukweli na uaminifu hakupenda unafiki.

Hayati Sokoine alifariki dunia kwa ajali ya gari mkoani Morogoro mwaka Aprili 12 mwaka 1984 akitokea Dodoma kuelekea mkoa wa Dar es Salaam.

Makinda aliyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati wa uchambuzi wa kitabu cha Hayati Sokoine ambacho kinatarajia kuzinduliwa Septemba 30 mwaka huu na Rais Samia Suluhu Hassan.

Kitabu hicho kitakuwa kinaelezea maisha ya Hayati Sokoine na uongozi wake kilichoandaliwa kwa kushirikiana na Taasisi ya Uongozi na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo.

Kinaangazia safari yake, kuanzia makuzi yake katika jamii ya Kimasai, kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi, ikiwemo kuwa Waziri Mkuu. Kinachangia kukuza historia ya Tanzania na Bara la Afrika kwa ujumla.

"Alitufundisha uaminifu na ukweli, hakuwa mnafiki kama umefanya kazi vizuri anakusifia, tuache unafiki na kujipendekeza kazi zetu zitatubeba kikubwa tuwe na matendo mema katika utekelezaji wa majukumu yetu,”amesema Makinda.

Aidha, amesema Sokoine alifanya kazi kwa bidii na alikuwa mfuatiliaji wa shughuli zote za serikali alipendwa na wananchi mbalimbali wakiwemo wa hali ya chini.

Makinda amesema Februari 25 mwaka 1983 akiwa Waziri wa Nchi, katika Ofisi ya Waziri Mkuu aliwahi kufanya kazi kwa mwaka mmoja na hayati Sokoine aliyeku mstari wa mbele kukabiliana na wahujumu uchumi.

"Kutokana na mapambano haya makubwa wananchi wa kawaida walimpenda kwa sababu alijali watu ndiyo maana akienda nyumbani kwake Monduli wamasai waliona gari lake ni la kwao," amesema Makinda.

Baada ya uzinduzi, kitabu kitapatikana kwenye maduka ya vitabu na maktaba mbali mbali nchini, vile vile mtandaoni kupitia www.mkukinanyota.com.