NGO zasaidia kupunguza ndoa, ukeketaji wa watoto

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 11:26 AM Sep 25 2024
Ukeketaji.
Picha: Mtandao
Ukeketaji.

UWAPO wa taasisi na mashirika ya kutetea haki za watoto wilayani Tarime mkoani Mara, umesaidia kupunguza ndoa za utotoni na vitendo vya ukeketaji kwa wasichana, imeelezwa.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wlaya ya Tarime, Peragia Baron, alisema hayo jana alipozungumza na viongozi kutoka Mtandao wa Kutokomeza Ndoa za Utotoni (TECMN) unaounda zaidi ya mashirika 80 likiwamo la Msichana Initiative, walioko katika ziara maalumu wilayani hapa kutoa elimu kwa jamii kuwalinda watoto dhidi ya ndoa za utotoni. 

Alisema miaka ya nyuma hali ya ndoa za utotoni wilayani hapa ilikuwa juu kwa sababu watoto wengi walikuwa wanaozwa wakiwa wadogo baada ya kukeketwa. 

"Ndoa za utotoni zipo na zinaendelea na zamani mtoto alikuwa akifika darasa la nne, analipiwa mahari na inaeleweka kabisa kwamba ni mke wa mtu na akiifika darasa la saba anaolewa,” alisema. 

Alisema kwa desturi za wakazi wa Tarime, mtoto akitahiriwa au kukeketwa huhesabiwa ni mtu mzima, hivyo anafaa kuoa au kuolewa.  

"Sasa hivi hizo  ndoa za utotoni bado zipo lakini si kwa kiwango kikubwa sana kama ilivyokuwa miaka ya nyuma. Kuna  baadhi ya sababu zilizochangia kupungua ikiwamo ujio wa vituo kwa taasisi za kutetea haki za binadamu vinavyosaidia kulea watoto wanaokimbia kuozwa kama hivi vya Masanga. 

"Kwa hiyo napendekeza kuongezeka kwa mashirika kama haya hata huko vijijini ili wafikiwe na elimu hii, kwamba programu zinazotolewa na mashirika haya zikifika kila kijiji, kwa asilimia kubwa tunaweza kuwaokoa wasichana wasiingie kwenye ndoa hizo za utotoni kwa sababu wengi hawana elimu huko na hawajui wakatoe taarifa wapi," alisema.  

Baron alisema maeneo yanayoongoza kwa kasi kwa mimba za utotoni na ukeketaji ni ya mipakani kama Sirari na Nyamongo ambayo yana shughuli nyingi za biashara ya madini. 

Alisema sababu kubwa kinachochangia mimba za utotoni katika wilaya hiyo ni vitendo vya ukeketaji na kwamba inapofika msimu wa ukeketaji kituo cha Masanga huwa kinaelemewa kutokana  na kupokea wasichana wengi wanaokimbia kukeketwa. 

Baron alisema kila mwaka wamekuwa wakitenga bajeti maalumu kwa idara ya ustawi wa jamii kwa ajili ya uelimishaji kuhusu kupambana na vitendo hivyo vya ukeketaji na ndoa za utotoni. 

Lilian Kimati, Mratibu wa Mtandao wa Kutokomeza Ndoa za Utotoni Tanzania, alisema lengo la kutoa elimu hiyo wanatamani ndoa hizo ziishe ili watoto wapate fursa ya kutimiza ndoa zao. 

"Ndiyo maana tumekuwa tukipigania sana mabadiliko ya sheria ya ndoa ambayo inatoa mwanya kwa watoto wadogo kuolewa, tunaamini hii ikifanyiwa mabadiliko huenda ndoa hizi za utotoni ikabaki historia,” alisema.

 Hivi karibuni Shirika la Msichana Initiative lilieleza kusikitishwa kwake kutokana na kukwama kwa mchakato wa kufanyia mabadiliko vifungu vya 13 na 17 vya sheria ya ndoa ya mwaka 1971 vinavyoruhusu mtoto wa miaka 14 kuolewa. 

Valerian Mgani, Meneja Miradi wa Association for Termination of Female Genital Mutilation (ATFGM) Masanga wilayani Tarime, alisema juhudi zote wanazozifanya kupambana na ndoa hizo za utotoni wilayani humo zimekuwa zikikwamishwa na baadhi ya wanasiasa ambao wamekuwa wakitumia nguvu kubwa kuwalinda wale wanaotekeleza vitendo hivyo. 

"Sisi tunapofanya kazi kupambana na vitendo vya ukeketaji pamoja na ndoa za utotoni, tunaingia kwenye vita kali na baadhi ya wanasiasa, wao wanasema eti tunaingilia mila za wapigakura wao na hata tukiwapeleka polisi wanaona tunakwenda kinyume na taratibu zao, wanapambana kuwatoa," alisema Mgani. 

Kwa mujibu wa Utafiti wa Demografia na Afya (TDHS) wa mwaka 2015/16, asilimia 36 ya wasichana Tanzania  wanaolewa kabla ya kufikisha umri wa miaka 18 huku mikoa inayoongoza kwa ndoa hizo ikiwa ni Shinyanya asilimia 59, Tabora asilimia 58,   Mara 55 na Dodoma 51.