Polisi yachunguza kifo cha kijana aliyefariki akiwa katika matibabu

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 11:14 AM Sep 25 2024
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Justine Masejo.
Picha: Mpigapicha Wetu
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Justine Masejo.

JESHI la Polisi mkoani Arusha, limesema linachunguza kifo cha utata cha Johnson Josephat, maarufu kama Sonii (39), Mkazi wa Unga Limited, jijini hapa, anayedaiwa kufariki dunia, baada ya kutoroshwa na kundi la watu waliokuwa wakipinga kukamatwa kwake baada ya kufungwa pingu mkono mmoja.

Josephat alifariki dunia juzi akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru. 

Jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Justine Masejo, alisema Septemba 23, muda wa saa 11:30 jioni,  askari polisi ambaye hajatajwa jina wala namba yake ya kijeshi, alifika maeneo ya Unga Limited kwa ajili ya kumkamata mtu huyo kwa madai ya kuhusika kwenye tukio la kuvunja stoo na kuiba. 

“Lakini wakati wa ukamataji askari alifanikiwa kumvisha pingu mkono mmoja, ndipo lilipojitokeza kundi la watu na kumshambulia askari, kumkamata mtu huyo na  kumtorosha kwa kutumia pikipiki,” ilidai taarifa ya polisi iliyotolewa kwa umma jana. 

Kwa mujibu wa SACP Masejo, taarifa za awali zinaonesha kuwa katika harakati za kumtorosha mtuhumiwa huyo alianguka na baadaye ndugu walimpeleka hospitalini lakini alifariki.  

Uchunguzi wa tukio hilo unaendelea ili kubaini chanzo cha kifo hicho ikiwamo kuchukua hatua kwa waliohusika ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao. 

Mke wa marehemu, Nasra Bakari, akizungumza katika video iliyosambaa mtandaoni, alisema mumewe alimkuta amekanyagiwa kichwa chini na askari wawili wa polisi. 

Alipouliza chanzo chake, aliambiwa kuna mtu mmoja alikuwa amekamatwa na polisi kwa tuhuma za wizi wa compreser, na alimtaja marehemu kuwa ni mhusika. 

Alisema baada ya kutajwa na polisi kumkamata mumewe walianza kimshambulia akiwa na pingu mkononi hadi kupoteza fahamu. 

Kwa mujibu wa Nasra, walipomkimbiza Hospitali ya Rufani ya Mkoa ya Mount Meru, walikataliwa mgonjwa wao kutibiwa kwa sababu alikuwa na pingu mkononi.