Bodaboda zaidi ya 200,000 Dar kufundishwa huduma ya kwanza

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:15 PM Sep 24 2024
Mkurugenzi Mtendaji wa TBL, Michelle Kilpin, akizungumza na  vyombo vya habari wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Elimu na Mafunzo kwa Waendesha Pikipiki uliofanyika jijini Dar es Salaam leo.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi Mtendaji wa TBL, Michelle Kilpin, akizungumza na vyombo vya habari wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Elimu na Mafunzo kwa Waendesha Pikipiki uliofanyika jijini Dar es Salaam leo.

MADEREVA wa bodaboda zaidi ya laki mbili wa mkoani Dar es Salaam, wanafundishwa jinsi ya kutoa huduma ya kwanza kwa majeruhi na elimu ya usalama barabarani, kwa ajili ya usalama wao na watu wengine.

Elimu hiyo itatolewa na  Tanzania Breweries Limited (TBL), kwa kushirikiana na  Chama cha Msalaba Mwekundu (Tanzania Red Cross Society) (TRCS), na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani.

Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa Maendeleo ya matawi ya chama hicho nchini, Rehinald kutoka chama hicho, Reginald Mhango, wakati wa uzinduzi wa mpango wa kutoa elimu na mafunzo kwa madereva hao, jijini Dar es Salaam.

"Katika mpango huu wa kutoa elimu, tutatumia miezi mitatu hadi Desemba tukijikita pia  katika mafunzo ya udereva na sheria ya usalama barabarani ili kusaidia kupunguza ajali," amesema Muhango.

Amefafanua kuwa chama hicho kina uzoefu wa zaidi ya 50 katika kutoa huduma mbalimbali ndani ya jamii yanapotokea majanga.

"Lakini tumegundua kuwa kuna tatizo kwenye suala la huduma ya kwanza inapotokea ajali, hivyo tunakwenda kuwaelimisha ili wanapopata ajali au wakikuta mtu amepata ajali wajue jinsi ya kumhudumia kabla ya kumfikisha hospitali " amesema.

Mkurugenzi TBL, Michelle kilpin  ambaye kampuni yake imedhamini mafunzo hayo, amesema kampuni hiyo inatamani kupunguza ajali za barabarani, kwa kuwa wanaamini kwamba wanapopunguza ajali, wanaokoa maisha ya watu.

1
"Tunatamani kupunguza ajali za barabarani kwa asilimia 50 kupitia elimu Kwa madereva wa vyombo vya moto wakiwamo wa bodaboda," amesema Michelle na kuongeza kuwa;

"Tanzania Breweries Limited inaunga mkono lengo la maendeleo endelevu ya umoja wa kimataifa (SDG) la kupunguza kwa nusu ya idadi ya vifo na majeraha yatokanayo na ajali za barabarani ifikapo 2030. Tunaamini kampuni yetu ina fursa ya kipekee ya kuboresha usalama barabarani na kuleta mabadiliko chanya katika jamii zetu. Mpango huu wa usalama barabarani ni sehemu ya juhudi zetu za Kampeni ya Smart Drinking na kipaumbele kwetu kutokana na kwamba wenzetu, familia zao, na wateja wetu wanasafiri barabarani kila siku." amesema

"Waendesha pikipiki hawa watafikiwa kupitia vyama vyao vilivyopo kwenye wilaya nne za Dar es Salaam: Kinondoni, Ubungo, Ilala, na Temeke.Mpango huu utabuni na kutekeleza mtaala maalum, kuanzisha ushirikiano wa kimkakati na shule za uendeshaji, kushirikisha jamii kupitia warsha, na kuendesha kampeni za uhamasishaji" amesema

Mkuu wa mafunzo Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Dinah Mosy, amesema baadhi ya madereva wa bodaboda hawana nidhamu.

2
"Licha ya jeshi kujitahidi kuwaelimisha, baadhi yao hawazinhatii, wapo wanaojifunza usiku kuendesha pikipiki kisha asubuhi wanaingia barabarani abiria na kuhatarisha maisha yao na ya abiria.

Mwenyekiti wa shirikisho la madereva wa bodaboda na Bajaj Mkoa wa Dar es Salaam, Said Kagoma, ameomba wapunguziwe ada ya udereva ili iwe rahisi madereva wote kwenda vyuoni.

"Kusoma unatakiwa kulipa ada ya sh. 180,000, madereva wengi hawana kulipa kiasi hicho kwa, hivyo tunaomba kipunguzwa hadi kufikia sh 30, 000 kwa mwezi, kiasi hicho tunaweza kukimudu," amesema Kagoma