Polisi yadhibiti maandamano CHADEMA

By Waandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:06 AM Sep 24 2024
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akiwa chini ya ulizi wa polisi alipokamatwa eneo la Magomeni Mapipa jijini Dar es Salaam jana.

JESHI la Polisi nchini limefanikiwa kudhibiti maandamano ya viongozi na wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika maeneo mbalimbali Dar es Salaam.

Aidha, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Jumanne Muliro, alitaja viongozi na wanachama 14 waliokuwa wanashikiliwa kwa madai ya kukaidi katazo la polisi la maandamano lilitolewa Septemba 12, mwaka huu. 

Kamanda Muliro alisema jana kuwa mwezi huu, viongozi na wanachama wa CHADEMA walitoa matamko mbalimbali yenye viashiria vya uvunjifu wa amani na kujenga hofu kwa wananchi na kwamba walipanga kufanya maandamano jana ambayo yalipigwa marufuku na polisi. 

Aliwataja walioshikiliwa kuwa ni Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, Makamu Tundu Lissu, na Mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini na Mjumbe wa Kamati Kuu, Godbless Lema. 

Wengine ni Peter Lazaro, Sheikh Omari Fakhi, Revocatus Mlay, Paulo Musisi, Shabani Kinde, Abubakar Mugalu, Emmanuel Ntobi, Sylvester Satu, Rachel Mlondela, Mary Nungi na Bakari Salum. 

TAARIFA YA CHADEMA

Kutokana na tukio hilo, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mrema, alitoa taarifa kuwa viongozi wanane, walinzi na watumishi wa makao makuu waliokuwa ofisini na zaidi ya wanachama 40 wanashikiliwa na polisi.

Aliwataja wengine ambao hawatajatwa kwenye taarifa ya polisi kuwa ni Naibu Katibu Mkuu, Benson Kigaila, Mke wa Mbowe, Dk. Lilian Mtei, wakili na mtoto wa kiongozi huyo, Nicole Mbowe aliyekuwa ameongozana na baba yake.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mrema, wengine waliokamatwa ni wenyekiti wa mikoa ya Katavi na Shinyanga Rhoda Kunchela na Emmanuel na viongozi mbalimbali wa majimbo ya Kanda ya Pwani.

“Tunatoa wito kwa Jeshi la Polisi kuheshimu katiba na sheria za nchi kwa kuwa kuandamana si kosa kwa mujibu wa katiba, sheria na taratibu zilizopo. “Pia tunalitaka Jeshi la Polisi kuheshimu haki zote za waliokamatwa na kuwatendea kama watu ambao si wahalifu kwa wakati wote wa kushikiliwa kwao,” alisisitiza.

Awali, alisema chama hicho kilitangaza kuwa jana ingekuwa siku ya maombolezo juu ya viongozi, wanachama na wananchi mbalimbali ambao wametekwa, kuteswa, kuumizwa, kupotezwa na wengine kuuawa nchini.

“Pamoja na kufuata utaratibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa kifungu Cha 11(4) kuhusu kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi juu ya maandamano ya amani ambayo yalipangwa kufanyika Dar es Salaam. Polisi wameamua kutumia nguvu kupita kiasi kudhibiti maandamano hayo,” alisema Mrema.

WAANDISHI WAKAMATWA

Waandishi watano na wapigapicha wa magazeti ya Nipashe, Mwananchi,  walikamatwa na polisi katika maeneo mbalimbali wakitekeleza majukumu yao kwenye matukio ya maandamano.

Mpigapicha Jumanne Juma alikamatwa Kituo cha Mafuta Buguruni wakati akipiga picha wanachama wa CHADEMA waliokusanyika eneo hilo. 

Baada ya kukamatwa, alipelekwa Kituo cha Polisi Buguruni, ambako alihojiwa kwa saa moja kwamba kwa nini anapiga picha wakati hakuna maandamano.

“Nilipofika nilikwenda kujitambulisha kwa kiongozi wa askari waliokuwapo lakini baada ya muda walituzunguka wakatukamata mimi na mwandishi wa Mwananchi. Tukapelekwa  kituoni tukahojiwa, baadaye wakatupeleka kwa mkuu wa kituo ambaye aliwaambia kama wametuhoji na hatuna madhara tuachiwe ndipo tukaachiwa,” alisema Juma. 

Aidha, Mwandishi wa Nipashe, Jenipher Gilla, alikamatwa wakati akikusanya taarifa za maandamano hayo kisha kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi.

Akizungumza kituoni hapo, alisema alifikishwa kisha kuhojiwa kwa nini alikuwa anakusanya taarifa kwenye eneo hilo. Waandishi wengine waliokamatwa ni Michael Matemanga na Lawrence Mnubi wa Mwananchi na Mariam Shaban wa EATV.

WAANDISHI KUFUKUZWA 

Baada ya zogo la mwandishi, Mbowe na makada kutamatika palitulia kwa muda eneo hilo ilipofika majira ya saa 6:45 adhuhuri, Jeshi la Polisi lilianza kuwafukuza waandishi eneo la Magomeni Mataa ambako kamatakamata hiyo ilikuwa ikifanyika na kuamuru  waende wakakae upande wa pili uliko Msikiti wa Kichangani. 

Hata hivyo ulitokea ubishani mkali waandishi wakidai wananyimwa uhuru wa kuripoti maandamano hayo japo majibu ya Polisi yalikuwa "hapa hamna jipya tena mmeshaturekodi sana inatosha." 

Ubishani huo ulidumu kwa dakika kadhaa mpaka alipotokea mmoja wa askari ambaye aliwaondoa na kuwapeleka nyuma ya kituo cha mafuta  ambako isingekuwa rahisi kuona kinachoendelea mbele ya barabara.

 HALI ILIVYOKUWA 

Mbowe alifika eneo la Magomeni majira ya saa 4:00 asubuhi, kuangalia usalama wa eneo kwa kuwa ndipo maandamano yalipangwa kuanzia. Kabla  ya kufika eneo hilo, tayari askari polisi walikuwa wametanda kuanzia Magomeni Mataa, Mapipa hadi Usalama.

Mbowe alifika eneo hilo pasi na Polisi na waandishi waliokuwapo baada ya kujua  amefika akiwa katika gari ndogo, alimshtua mmoja ili awaite wengine azungumze nao. Wakati mazungumzo yakiendelea, polisi walimfuata na kumkamata huku wakimweleza aingie kwenye gari waondoke. 

Kabla ya kukamatwa, Mbowe aliwaambia waandishi wa habari kuwa maandamano hayo ni ya amani na lengo lao ni kuomboleza vifo vya makada wa chama hicho na kukemea mauaji na utekaji. 

"Hapa ndio tulipanga kuanzia maandamano yetu, maandamano yetu ni ya amani na hatuna nia ya kudhuru watu wala serikali. Kuna madai tuliyatoa kwa serikali hayajafanyiwa kazi, maandamano ni haki yetu kikatiba pale nguvu kubwa kama hii inavyotumika kukusanya askari wenye silaha na gharama kubwa kwa kutumia kodi za wananchi hii haiko sawa. 

"Nimelazimika kuja hapa Magomeni na niko tayari kwa lolote maandamano haya si ya CHADEMA tu bali kwa mtu yoyote anayechukizwa na vitendo vya mauaji na utekaji," alisema Mbowe.  

Wakati Mbowe anamalizia kauli yake maofisa wa Jeshi la Polisi walivamia mahojiano yake na kuanza kumzonga wakitaka aingie kwenye gari. Zogo hilo lilidumu kwa dakika kadhaa kisha Mbowe akashindwa kihimili mkikimikiki na kukubali kuingia katika gari dogo jeusi. 

Wakati anapeleka kuingizwa katika gari hilo alikuwa akitamka kwangu: "Haya ndiyo malipo ya kutetea demokrasia na mauaji, hii ndio gharama tunayolipwa katika nchi." 

Katika eneo la Mnazi Mmoja, ambako maandamano yalipangwa kupokewa yakitokea Magomeni na Ilala Boma, hali ilionekana kuwa shwari kuanzia majira ya saa 1:00 asubuhi wakati jua likichomoza hadi 7:00 mchana, huku kelele za magari na shughuli mbalimbali za wananchi zikitawala.

Katika barabara inayotoka Ilala Boma hadi Mnazi Mmoja, askari walionekana kutanda maeneo mbalimbali kama Karume na Kariakoo, huku kwa upande wa Magomeni walionekana Jangwani na Fire kuelekea katikati ya mji.

MAONI YA WANANCHI

Mwanaharakati Helen Kijo Bisimba alisema: “Nilikuwa bado natafakari kuwa kama taifa  hatutaki kuingiliwa mambo yetu  ya ndani, nikakumbuka tulivyokuwa mstari wa mbele kukemea yaliyokuwa yanaendelea Afrika Kusini kwa makaburu, Rodesia ya Kusini  na Kaskazini hadi Nigeria kule Biafra yale hayakuwa mambo ya ndani ya nchi zile? 

“Tumefika  mahali na sisi tunatenda mambo ambayo wengine hawawezi kunyamaza. Wapo wanaoingilia mambo yetu ya ndani  kwa kujenga zahanati ambazo ni kazi zetu hatukuwakataza, ila wakituonyesha ukweli wa maovu ya ukiukwaji haki, tunadai wanaingilia mambo yetu ya ndani. Tujirudi serikali ifanye masahihisho badala  ya kulaumu wanaowaambia ukweli.”

Richard Mabala aliandika: ”Serikali ilipewa wiki moja kujikita katika kuondoa sababu ya maandamano kwa kuonyesha umakini katika kukomesha utekaji na kuwakamata watekaji  au kujikita katika kuzuia maandamano kwa mabavu ya kila aina, inasikitisha sana kwamba waliamua kujikita katika ya pili.”

Manyerere Jackton aliandika: “Hutakiwi kuwa mfuasi  wa chama cha upinzani kuamini kuwa maandamano ya amani ni haki ya kiraia, na kwamba  kuandamana ni sawa na kufungua chupa iliyojazwa chai ya moto! 

“Watu wakiandamana wanapumua. Hakuna sababu ya kutumia gharama kubwa kuzuia haki za kiraia, maandamano ya kweli hayapo barabarani  bali yako  vichwani na  mioyoni mwa watu, je, nani wa kuyazuia maandamano yaliyo mioyoni mwa watu? Tuione na tuifanye Tanzania kuwa ni yetu sote Amani Daima.”

Imeandikwa na Halfani Chusi, Maulid Mmbaga, Jenipha Gilla na Grace Mwakalinga.