RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema serikali kwa kushirikiana na Watanzania waishio nje ya nchi (diaspora) wamepanga kufungua vituo 100 vya lugha ya Kiswahili kwenye maeneo mbalimbali duniani.
Aidha, vijana wabunifu wametakiwa kutumia mbandiko (Application) mbalimbali kwa ajili ya kufundisha Kiswahili kupitia mitandao ambayo itawafikia wananchi wengi.
Samia alitoa kauli hiyo jana, akifunga kilele cha Tamasha la Kitaifa la Utamaduni lililofanyika katika mji wa Songea, mkoani Ruvuma, akiwataka Watanzania waishio nje pamoja na vijana, kuchangamkia fursa zitakazopatikana kupitia lugha hiyo.
Aliwataka vijana watumie ubunifu kwa kutengeneza maigizo na teknolojia nyingine ili kuyafikia mataifa mengine kujifunza Kiswahili ambacho kwa sasa kinatoa ajira na fursa mbalimbali za kiuchumi.
Aidha, alisema njia nyingine ya kusaidia lugha hiyo ni kutambulika zaidi duniani na vyuo vikuu nchini kushirikiana na vyuo vya nje kuhamasisha kutumia lugha hiyo.
“Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo imenijulisha kwamba mwaka huu imepanga kufungua vituo 100 vya Kiswahili kote duniani kwa kushirikiana na diaspora yetu, niwatake Watanzania waliopo nje ya nchi kuchangamkia fursa ya kufundisha Kiswahili, pia vijana kupitia ubunifu wa maagizo na mtandiko watu watavutika kutaka kuifahamu lugha hiyo nanyi mtajiingizia kipato alisema,” alisema.
Katika hatua nyingine, Rais Dk. Samia, aliiagiza Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo kuandaa mapendekezo ya kushughulika na masuala ya mmomonyoko wa maadili.
Alisema mapendekezo ya wizara yataisaidia serikali jinsi ya kupambana na mmomonyoko wa maadili ambao alisema umetokana na mwingiliano wa utamaduni wa kigeni na kuwataka wazazi na walezi kukagua mwenendo na maadili ya watoto wao.
Awali, Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, Damas Ndumbaro, alimweleza Rais Samia kuwa ni msimu wa tatu Tamasha la Kitaifa la Utamaduni linafanyika na kwa mara ya kwanza lilikuwa Septemba 8, 2021, la pili lilifanyika mkoani Njombe na sasa limefanyika Ruvuma.
Alisema tamasha hilo linajitahidi kutimiza falsafa za Rais Samia ambazo ni maridhiano kwa kuhusisha makabila yote kubadilisha mawazo na kutatua migogoro katika sekta ya utamaduni, sanaa na michezo kwa kuzingatia maridhiano.
Kuhakikisha sekta ya michezo inachangia Pato la Taifa kutoka asilimia 0.4 hadi kufikia nne, kujenga upya, kutetea maadili na kukuza sekta ya muziki na sanaa.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, alisema wamenufaika na miradi mbalimbali ya maendeleo kama vile sekta ya afya, kilimo, elimu na nishati, hadi sasa zaidi ya vijiji 500 vimeunganishwa na umeme.
Rais Samia ambaye ameanza ziara ya siku sita mkoani Ruvuma kwa ajili ya kukagua miradi ya maendeleo, alisema kuwa tangu iingie madarakani mwaka 2021 serikali imetoa fedha nyingi kujenga shule, hospitali, maji, barabara, kuboresha sekta ya madini na kilimo.
Alisema ameridhishwa na upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Songea kilichogharimu Sh. bilioni 40.
Pia, kiwanja hicho kimeboreshwa na kina uwezo wa kushusha abiria kutoka 3,000 katika mwaka 2021 hadi kufikia 1920, mwaka huu.
Imeandikwa na Grace Mwakalinga (DAR) na Gideon Mwakanosya (RUVUMA)
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED