"Tuunge mkono kwa vitendo mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya kupikia"- Katimba

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:05 AM Sep 24 2024
"Tuunge mkono kwa vitendo mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya kupikia"- Katimba

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Zainabu Katimba ametoa rai kwa wananchi kuunga mkono kwa vitendo Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ambayo ni Ajenda iliyoanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan.

"Nyakati zimebadilika, tuunge mkono juhudi za Mheshimiwa Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan katika matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kutumia nishati safi kama gesi, umeme na nyinginezo. " amesema Katimba

Ameongeza kuwa, watanzania wanapaswa kuwa sehemu ya Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia na kuonesha mabadiliko kwa vitendo kwa kutoka kwenye matumizi ya nishati zisizo safi na salama.

Aidha, amesisitiza kuwa, matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia yatapunguza kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira  ambapo takwimu zinaonesha kila mwaka takribani hekta 469,000 za msitu zinateketea kwa sababu ya shughuli mbalimbali za kibinadamu ikiwemo matumizi ya nishati zisizo safi za kupikia (kuni na mkaa).

"Tukitumia Nishati Safi ya Kupikia hatutaokoa mazingira peke yake bali  afya za watu pia kwani  takribani watu 33,000 hupoteza maisha kwa sababu ya matumizi ya nishati zisizo safi, hii ni kutokana na mazingira ya jikoni ya moshi, hewa nzito ambayo huleta athari katika  mfumo wa upumuaji." ameongeza Katimba

Kuhusu mtazamo wa kuwa  gesi inayotumika majumbani kupikia inalipuka, Katimba amesema kuwa gesi hiyo ni salama kwa matumizi husika.