1,800/- zilivyowezesha watoto kupata mchele, nyama, mafuta

By Waandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:39 AM Sep 25 2024
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan akipokea zawadi ya pesa kutoka kwa mmoja wa wanafunzi wa Shule ya Awali na Msingi ya Mchepuo wa Kiingereza ya Chief Zulu, baada ya kuizindua shule hiyo, mjini Songea mkoani Ruvuma jana.
PICHA: IKULU
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan akipokea zawadi ya pesa kutoka kwa mmoja wa wanafunzi wa Shule ya Awali na Msingi ya Mchepuo wa Kiingereza ya Chief Zulu, baada ya kuizindua shule hiyo, mjini Songea mkoani Ruvuma jana.

KATIKA hali isiyotarajiwa, wanafunzi wa awali katika Shule ya Msingi ya Mchepuo wa Kiingereza ya Chief Zulu, katika Mtaa wa Namanyigu Kata ya Mshangano, Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, walimpa Rais Samia Suluhu Hassan Sh. 1,800 walizochanga kwa nyakati tofauti.

Baada ya Rais Samia kufika shuleni hapo, mwanafunzi mmoja alikwenda moja kwa moja na kumpa Sh. 50.

Akisimulia tukio hilo ambalo alionyesha lilimgusa, Rais Samia alisema mwanafunzi alipokea fedha hiyo kisha akamrudishia lakini baada ya kutafakari, aliamua kumtafuta na kuipokea tena.

“Nilivyomtafuta nikampata nikamwambia nipe ile pesa uliyotaka kunipa. Akanipa kisha nikaona wanafunzi wenziwe nao wanakuja kunipa Sh. 50 na 100. Nilipohesabu baadaye nikajikuta nina Sh. 1,800,” alisema.

Rais Samia alisema alimchukulia mtoto huyo kama malaika aliyekwenda kumpa baraka, ndiyo sababu iliyomsukuma kumtafuta na kuzipokea fedha zote. Alisema  hali hiyo ilimfurahisha na kumtafakarisha, hivyo kuamua kuwapa ng’ombe wawili, mchele kilo 500 na mafuta ya kupikia.

"Sasa hizi fedha nakwenda kuziweka kwenye makumbusho yangu na maandishi maalum ya watoto hawa. Kama wajukuu, wamepata fikra ya kunigawia mimi bibi. Kwa  nini mimi bibi nisiwagawie wao," alisema. 

Rais aliwahimiza walimu wa shule hiyo wawatunze na kuwalinda watoto hao na majengo ili yaendelee kuwa na hali hiyo na kuvutia kwa muda mrefu.

MAZAO YA BIASHARA

Akiweka jiwe la msingi la  ujenzi wa maghala 28 ya kuhifadhi nafaka katika kijiji cha Luhimba, Rais aliwakumbusha wakulima kuwa na matumizi mazuri ya fedha ili soko la mazao linaposhuka wasiathirike kiuchumi.

Aliwakumbusha wakulima wa kahawa kuongeza jitihada katika uzalishaji ili kukuza uchumi na hatimaye serikali ijiepushe na misaada na mikopo yenye masharti.

Rais pia aliweka jiwe la msingi katika mradi wa maji wa Mtyangimbole, kijiji cha Madaba na kutembelea shamba la kahawa la Aviv Tanzania, kijiji cha Lipokela.

Akiwa kijijini hapo, Rais aliwasihi wakulima wa mazao yote nchini kuwa na mipango mizuri ya matumizi ya fedha ili wasishuke kiuchumi kwa kuwa soko la mazao lina tabia ya kupanda na kushuka.

“Kwa hiyo niwaombe sana wakulima wote, misimu ikiwa mizuri bei ikiwa nzuri, tujue kujiwekea akiba ili mabadiliko ya tabianchi yakituathiri, mvua zisipokuja, bei zikishuka, tusitetereke kiuchumi na hali za maisha,”  alisema.

Rais aliwasihi wakulima wa kahawa  kuongeza kasi ya uzalishaji ili nchi ijitegemee kwa kuwa fedha zinazotumika kuboresha sekta ya kilimo, likiwamo zao hilo.

Alisema kama nchi itakuwa na uwezo wa kuzalisha dola milioni 250 na zaidi kwa  kahawa pekee, huku wakulima wakiongeza juhudi na kuzalisha zaidi, nchi itaondokana na mikopo yenye masharti.

“Tunapotaja dola milioni 250 ndugu zangu, huwa nakwenda nje napiga magoti, nabembeleza na kuomba na wakati mwingine kwa masharti,” alisema.

Rais alimwagiza Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, kushughulikia malalamiko ya wananchi ya kukatwa fedha kinyemela na vyama vikuu vya ushirika na kuweka mfumo wa uwazi ili wanufaike na mazao yao.

Pia aliwakumbusha wakulima wa kahawa wazingatie uhifadhi wa mazingira ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazosababisha mvua kutotabirika ili wawe na uhakika katika uzalishaji wa mazao yao.

Rais Samia aliitaka Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) kufuata masharti yanayayotolewa na soko la Ulaya ya kutokukata misitu kwa ajili ya kulima kahawa kwa kuwa wakifanya hivyo, zao hilo halitanunuliwa.

Alisema Umoja wa Ulaya (EU) ulielekeza kuwa mashamba yote mapya yatambuliwe na kusajiliwa katika soko la dunia ili kufahamu kahawa imetoka mashamba yapi na kama kuna uharibifu wowote wa mazingira.

“Hili nalo si la kupuuza. Naomba  twende nalo tuliandikishe ili tusije tukakosa soko zuri la kahawa kule Ulaya,” alisema.

Rais alielekeza teknolojia ya visima  vya umwagiliaji, kilimo cha pilipili manga na paprika  iliyoko kwa mwekezaji ipelekwe  kwa wananchi ili nao waitumie kwenye kilimo na kujiongezea kipato.

Pia alisema tangu nchi ipate uhuru, serikali imeanza kutoa ruzuku kwenye zao hilo hali iliyosababisha kuongezeka kwa uzalishaji kutoka tani 65,000 hadi 80,000 nchi nzima na kuongeza kipato kupitia fedha za kigeni na mwaka huu, mauzo ya kahawa yanatarajia kuingiza dola milioni  250.

Alisema katika kipindi cha miaka mitatu, serikali ilipunguza makato ya tozo na ushuru, ukiwamo ushuru wa halmashauri  kutoka asilimia tano hadi tatu ili mkulima afurahie kazi ya mikono yake.

SERIKALI ZA MITAA

Akiwa Peramiho, Rais Samia aliwasisitiza wananchi kujitokeza kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba, mwaka huu, kugombea nafasi mbalimbali na kuwachagua viongozi wanaofaa.

Aliwasihi kuchagua wagombea wa Chama Cha Mpinduzi (CCM) kwa sababu serikali yake inawajibu wa kuhakikisha nchi inabaki salama na utulivu wa kisiasa na kuwaletea maendeleo.

Rais pia aliwataka Watanzania kudumisha amani, utulivu na usalama katika maeneo yao kwa kuwa ndio msingi wa maendeleo ya nchi na kuahidi kuwa serikali itaendelea kuwaletea maendeleo.

Aliwaeleza Masista wa Shirika la Masista Wamisionari Wabenediktini wa Tutzing kudumisha upendo kwa watu wote bila kuangalia utofauti za dini kwa kuwa binadamu wote ni sawa na hakuna mtu aliyeumbwa tofauti na mwenzake.

Waziri wa Kilimo, Bashe alisema  kuwa  ujenzi wa maghala 28 Luhimba ni sehemu ya kwanza ya utekelezaji wa maelekezo  ya Rais Samia ya kujenga maghala 70 vijijini yenye  uwezo wa kuhifadhi tani 1000 kila mojawapo yatakayogharibu Sh. bilioni 14.7 sawa na Sh. milioni 527 kwa kila ghala.

Alisema kuwa maghala hayo yamejengwa katika Halmashauri za Wilaya za Songea Manispaa na idadi ya magahala kwenye mabano ni Songea Mji, Songea DC (11), Madaba (9) na Namtumbo (saba).

Bashe alisema maghala mengine ni Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) matano kuhudumia wakulima na kati ya 28, mengine matano yanatarajiwa kukamilika wiki chache zijazo.

Alisema NFRA pia itajenga maghala makubwa ya kisasa yenye uwezo wa kuchukua tani 5,000 kila ghala katika mikoa ya Katavi, Rukwa, Ruvuma, Songwe na Tabora.

TAMISEMI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, alisema ujenzi wa Shule ya Msingi Chief Zulu uliogharimu  Sh. milioni 626.43 ulibuniwa na madiwani wa halmashauri hiyo.

Awali, Waziri wa Afya na Mbunge wa Peramiho, Jenista  Mhagama, alimwomba Waziri Bashe aongeze miradi ya umwagiliaji ili kuboresha mazao ya kilimo cha biashara katika eneo hilo.