TAMISEMI yatakiwa kuwasilisha kiapo kinzani siku 14 mahakamani

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 11:20 AM Sep 25 2024
TAMISEMI yatakiwa kuwasilisha kiapo kinzani siku 14 mahakamani
Picha: Mtandao
TAMISEMI yatakiwa kuwasilisha kiapo kinzani siku 14 mahakamani

MAHAKAMA Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, imetoa siku 14 kwa upande wa Jamhuri kuwasilisha kiapo kinzani katika kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na wanaharakati watatu kupinga Wizara Ofisi ya Rais Tawala za Mkoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024.

Mahakama hiyo ilifikia uamuzi huo, baada ya kutoa kibali kwa Mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA), Bob Wangwe, Mwenyekiti wa JUKATA, Dk. Annanilea Nkya na Bubelwa Kaiza cha kuwasilisha mapitio ya mahakama (Judicial review) ili kutekeleza haki kwa mujibu wa sheria na kanuni.

Kesi ilitajwa jana mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu, David Ngunyale, jopo la mawakili wa serikali liliomba lipewe siku 14 kuwasilisha kiapo kinzani kwa ajili ya kujibu hoja zilizowasilishwa na wanaharakati hao kupitia mawakili wao Mpare Mpoki na Jebra Kambole.

Hata hivyo, Wakili Mpoki na Kambole walipinga hoja hiyo kwa madai kuwa wamewasilisha mapitio hayo chini ya hati ya dharura, kwa upande wao siku hizo ni nyingi.

Jaji Ngunyale alikubaliana na ombi la upande wa Jamhuri la siku 14 na kuahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 7, mwaka huu, kwa ajili ya kutajwa, kama kila kitu kitakuwa kimewasilishwa kwa wakati mahakamani hapo, basi kesi itasikilizwa.

Wanaharakati hao, wamefungua kesi hiyo dhidi ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Wangwe na wenzake wanapinga uchaguzi huo kusimamiwa, kuratibiwa na kundeshwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI, badala yake Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kwa mujibu wa Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi ya mwaka 2024.

Pia, wanapinga kanuni za uchaguzi huo za mwaka 2024 zilizotungwa na Waziri wa TAMISEMI, wakihoji mamlaka yake ya kutunga kanuni hizo.

Awali, mahakama hiyo ilikataa kutoa zuio la utekelezaji wa mchakato wa uchaguzi unaoendelea hivi sasa kwa sababu waleta maombi hawakuweka hoja hiyo kwenye kiapo chao wala kwenye maelezo yao ya shauri walilokuwa wamefungua.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 umepangwa kufanyika Novemba 27. 

Agosti 15, 2024 Waziri wa TAMISEMI alitangaza kuanza kwa mchakato wa uchaguzi huo kuanzia tarehe hiyo hadi Novemba 27, mwaka huu.