Mahakama Kuu yatengua hukumu ya Mahakama ya Kisutu malipo mil. 100/-

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 12:49 PM Mar 28 2024
Mahakama Kuu ya Tanzania
PICHA: Maktaba
Mahakama Kuu ya Tanzania

MAHAKAMA Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, imetengua hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliyomtaka mfanyabiashara Sudhir Lakhanpal kumlipa aliyekuwa Mkurugenzi mwenza, Azim Hooda, Sh. milioni 100 alizokopeshwa.

Jaji John Nkwabi alifikia uamuzi huo baada ya kukubali rufaa iliyowasilishwa na mrufani Lakhanpal, kupinga uamuzi wa Mahakama ya Kisutu ambayo ilikubali maombi ya mjibu rufaa Hooda.

Jaji Nkwabi alisema, ameridhika kuwa Mahakama ya Kisutu ilifanya makosa kumpa mjibu rufani Sh. milioni 100, na hukumu na amri ya mahakama hiyo inatupiliwa mbali.

Jaji huyo alibainisha kuwa hakuwa na uhakika ni lini hasa mrufani aliomba mkopo na hakukuwa na ushahidi wa kutosha kuthibitisha kuwa mrufani aliomba mkopo huo kutoka kwa mjibu rufaa.

"Nimeridhika kuwa kesi ya mjibu rufani ilikuwa na mikanganyiko isiyoweza kusuluhishwa katika ushahidi wa kila shahidi wake na jumla ya ushahidi uliotolewa wakati wa kusikilizwa shauri hili na Mahakama ya Kisutu," alisema Jaji Nkwabi.

Alisema kuwa shahidi mmoja alionesha kuwa fedha hizo zilikabidhiwa kwa mrufani ndani ya muda mfupi, lakini ushahidi mwingine unaeleza kuwa ilichukua zaidi ya miezi saba.

Pia, alibainisha kuwa mjibu rufani anadai kuwa ni rafiki wa mrufani, lakini inaonekana alikuwa na undugu na mjibu rufani kupitia Kampuni ya Regalia.

"Inahitaji ushahidi kwa mtu kukubali kwamba mtu anayefanya kazi katika taasisi moja ni rafiki wa mwingine, kwa sababu si kawaida kwamba kila mtu anayefanya kazi katika taasisi moja ni marafiki," Jaji alisema.

Wakati wa kusikilizwa kwa rufani hiyo, wakili wa upande wa mrufani, Joseph Rutabingwa, alisema kuwa ikiwa kweli mjibu rufani alitoa mkopo kwa mrufani, kwanini alitoa maelezo yanayokinzana kuhusu tarehe na awamu mbele ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Kisutu.

Kwa upande mwingine, mjibu rufani alidai kuwa mrufani kupokea kiasi hicho cha mkopo wakati anafanya kazi katika kampuni yake inayoitwa Regalia Tanzania Limited kama mkurugenzi na hajawahi kulipa.

Ilidaiwa kuwa mjibu rufani alimshtaki mrufani kwa madai ya aina mbalimbali, ikiwa ni pamoja na malipo ya Sh. milioni 100 kama mkopo uliotolewa kwake kwa kuwa walikuwa wanafahamiana na marafiki wa karibu.