Kawaida ataka viongozi kusikiliza wananchi

By Christina Haule , Nipashe
Published at 12:49 PM Feb 06 2026
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Morogoro, Josephat Masunga

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Mohamed Kawaida, amewataka viongozi na watendaji wa chama na serikali nchini kutenga muda wa kutosha kuwatembelea wananchi, kuwasikiliza na kutatua kero zao, badala ya kuendelea kukumbatia kero wanazojua wazi kuwa hawana uwezo wa kuzitatua.

Kauli hiyo imetolewa Februari 5, 2026, kupitia hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Morogoro, Josephat Masunga, wakati wa maadhimisho ya miaka 49 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) yaliyofanyika kimkoa katika eneo la Igima, Kata ya Mbingu, Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro.

Kawaida amesema uzoefu unaonesha kuwa mara nyingi wananchi huwasilisha kero zao kwa viongozi, lakini baadhi hazitatuliwi kwa wakati, huku nyingine zikifikishwa kwenye ngazi husika ilhali mhusika anayezipokea anafahamu hana uwezo wa kuzitatua. Ameeleza kuwa hali hiyo husababisha kero hizo kuendelea kukaa muda mrefu na wakati mwingine kuibua migogoro isiyokuwa ya lazima.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dunstan Kyobya, amesema mkandarasi wa barabara kuanzia Ifakara hadi Igima yupo kazini, huku serikali ikiendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili wananchi waweze kutumia fursa zilizopo kukuza uchumi wao.

Naye Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Emmanuel Ndyamukama, amewaomba wananchi kuitunza miundombinu inayojengwa na kuacha tabia ya kutupa taka kwenye mitaro inayojengwa sambamba na barabara.

Ameeleza kuwa barabara adui yake mkubwa ni maji, na kwamba licha ya maji kuwa uhai kwa binadamu, yakikutana na mitaro, madaraja au makaravati yaliyoziba husababisha mafuriko na uharibifu mkubwa wa miundombinu, hali inayoongeza gharama za ujenzi na matengenezo ya barabara.

Kwa upande mwingine, Meneja wa Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA), Mhandisi Sospeter Lutonja, amesema jitihada zinazochukuliwa na serikali ndizo zinazowawezesha watendaji kuingia kazini na kutekeleza miradi ya maji kwa ufanisi, jambo lililowafanya kuendelea kupata pongezi.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA), CPA Sais Kejo, amesema CCM imefanya kazi kubwa ya kuhakikisha maeneo mengi yanapata huduma muhimu ya maji safi na salama, akisisitiza kuwa jamii haina budi kutambua na kuthamini jitihada hizo, hususan wakati wa maadhimisho ya miaka 49 ya kuzaliwa kwa chama hicho.