RAIS Samia Suluhu Hassan amesema atalipia gharama za matibabu ya mtoto Maliki Hashimu (5), mkazi wa Goba, mkoani Dar es Salaam, anayedaiwa kujeruhiwa koo na mfanyakazi wa ndani (house girl).
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu aliyasema hayo jana baada ya kutembelea Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), jijini Dar es Salaam ambako mtoto huyo yuko chini ya uangalizi maalum.
Tukio la kujeruhiwa mtoto huyo kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, lilitokea usiku wa Julai 15 mwaka huu na kuripotiwa siku iliyofuata.
Kutokana na majeraha makubwa aliyopata baada ya kukatwa na kitu chenye ncha kali shingoni kilichotenganisha njia ya hewa chini ya sanduku la sauti, mtoto huyo alifikishwa MNH - Mloganzila.
Baadaye mtoto huyo alihamishiwa MNH - Upanga kwa ajili ya matibabu zaidi kwa kuwa baada ya kujeruhiwa kulisababisha ashindwe kupumua, kuongea na kupata maumivu na kupoteza kiwango kikubwa cha damu.
MNH kupitia wataalamu wake tayari wamemfanyia upasuaji mkubwa mtoto huyo, ukichukua saa nne kurekebisha njia ya hewa, sanduku la sauti, matezi yaliyojeruhiwa na kutibu jeraha la nyuma ya shingo.
Wataalamu hao walibaini jeraha la mbele ya shingo liliharibu tezi la mbele (thyroid gland) kwa kulikata katikati na kusababisha mtoto huyo kuvuja damu kwa wingi, kupata maumivu makali kutokana na kukatwa sehemu iitwayo (trachea) ambako hewa hupita inapotoka katika mapafu.
Tangu Jumatatu iliyopita, mtoto huyo yuko chini ya uangalizi maalum akiendelea kupata matibabu kutoka kwa madaktari bingwa wa hospitali hiyo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED