Daraja jipya nafuu usafiri, usafirishaji Ngerengere

By Christina Haule , Nipashe
Published at 01:09 PM Feb 04 2026
Daraja jipya nafuu usafiri, usafirishaji Ngerengere

Ujenzi wa daraja la upinde wa mawe pamoja na barabara ya Ngerengere–Sinyaulime yenye urefu wa kilometa 30 umetajwa kuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa Kata ya Ngerengere, kwa kuwaondolea adha ya usafiri na usafirishaji iliyokuwa ikidhoofisha shughuli za kiuchumi, baada ya daraja la awali kusombwa na maji kufuatia mafuriko makubwa ya mwaka 2024.

Akizungumza wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Morogoro iliyokuwa ikikagua miradi ya barabara wilayani Morogoro, Diwani wa Kata ya Ngerengere, Kibena Kingo, amesema ujenzi wa daraja hilo ni suluhisho la kudumu kwa changamoto zilizokuwa zinawakabili wananchi, ikiwemo kushindwa kuvuka mto na kukatika kwa mawasiliano kati ya pande mbili za kata hiyo.

Ameeleza kuwa adha hiyo ilisababisha tukio la kusikitisha mwaka 2024, ambapo mwalimu mmoja alishindwa kuvuka mto kwenda nyumbani kwake Ngerengere kwa siku mbili mfululizo, hivyo kushindwa kumnyonyesha mtoto wake mwenye umri wa miezi miwili kutokana na maji kujaa mtoni.

Kwa upande wake, mkazi wa Kijiji cha Sinyaulime, Shabani Ramadhani, amesema kwa muda mrefu wananchi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ya usafiri na usafirishaji, hususan nyakati za mvua, baada ya daraja la awali kusombwa na maji, hali iliyosababisha kukatika kwa mawasiliano, kuhatarisha maisha ya wananchi na kudhoofisha shughuli za kiuchumi.

Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Emmanuel Ndyamukama, amesema ujenzi wa daraja kwa mfumo wa upinde wa mawe ni imara na utawezesha daraja hilo kupambana na magogo makubwa yanayobebwa na maji wakati wa mvua kubwa.

Amesisitiza kuwa mkandarasi anapaswa kukamilisha ujenzi huo kwa haraka, akibainisha kuwa hakuna muda wa ziada utakaoongezwa katika utekelezaji wa mradi huo, ili wananchi waondokane na adha waliyozoea kuipata.

Aidha, ameipongeza Serikali kwa kuchukua hatua za haraka kwa kutenga Shilingi milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo lenye midomo miwili ya kupitishia maji, sambamba na uchongaji wa barabara yenye urefu wa kilometa moja.

Ameongeza kuwa mradi huo unalenga kurejesha mawasiliano ya uhakika pamoja na usalama wa usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa eneo hilo, ambapo umefikia asilimia 80 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika ifikapo Aprili 8, 2026.

Katika mradi huo, amesema shughuli zitakazotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa kuta za daraja, uchongaji wa barabara, uwekaji wa kifusi, ujenzi wa kingo za daraja pamoja na kubomoa daraja la zamani ili kuhakikisha daraja jipya linakuwa imara, salama na la kudumu.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Josephat Masunga, amewahimiza wakandarasi kuhakikisha wanatekeleza miradi kwa weledi na kutimiza makubaliano yaliyowekwa, ili fedha zinazotolewa na Serikali ziwe na thamani halisi kwa kuzingatia viwango na ubora unaotakiwa.

Naye Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Patrick Rambika, amesema ujenzi wa madaraja na barabara ya Ubena Zomozi hadi Ngerengere yenye urefu wa kilometa 11.6 una thamani ya Shilingi bilioni 20.5, ukiwahusisha madaraja makubwa mawili pamoja na boksi kalvati 11.