WAKATI majina ya wateule wa kuwania nafasi mbalimbali katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu yanatarajiwa kuwekwa hadharani kesho, baadhi ya vyama vya upinzani vimeendelea kulia na rafu kwa wagombea wao.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema hakitakubali kuona wagombea wake wakienguliwa, huku ACT-Wazalendo kikidai kuwa na taarifa za wagombea wake kurubuniwa na wasimamizi wa uchaguzi katika maeneo mbalimbali nchini.
Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Pwani, Boniface Jacob, amesema leo kuwa hawapo tayari kurudi nyumbani kufuta machozi ‘kuomboleza’ kwa wagombea wake kuenguliwa kwa sababu ambazo ni nje ya zile za kikatiba ambazo mgombea anatakiwa kuwa nazo.
"Safari hii hatususi, hatukimbii wala hatuliilii ovyo, hiari ni yao pawe na uchaguzi au pasiwe na uchaguzi. Kesho (leo) ni siku ya uteuzi, wanachama wetu, viongozi na wagombea tukusanyike tangu asubuhi kwenda kuangalia majina kama tumeteuliwa au haujateuliwa. Kama hatujateuliwa tusirudi nyumbani.
"Tumtafute mteuaji tukamhoji, kwa lolote ambalo litakuwa limeandikwa katika ubao, ninyi nyote ni mashahidi, hakuna mgombea ambaye amejaza fomu peke yake, wote wamejaza chini ya wanasheria Kanda ya Pwani mpaka zinarudishwa," amesema.
Jacob pia amewaonya wagombea wa chama hicho ambao wanapanga kufanya hujuma kwa kujitoa katika uchaguzi huo baada ya kuteuliwa, akisisitiza kuwa sababu pekee ya chama hicho kukosa mgombea ni kifo na si vinginevyo.
"Tumekupa nafasi kwa kukuheshimu na kukuona unatosha kugombea eneo hilo na wewe tuheshimu. Kila mtu ana tamaa, kila mtu ana njaa. Njaa zako funga breki. Kama ulichukua fomu ukataka kugombea, ukifikiri nafasi hiyo ni ya biashara, biashara hiyo ni ya hatari, acha!" Jacob ameonya.
Msemaji wa ACT-Wazalendo wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Rahma Mwita, amedai makada wa chama kimoja cha siasa nchini wanawalaghai wagombea wao ili wajiengue.
Amedai wanao ushahidi wa vitendo hivyo katika baadhi ya maeneo, yanayojumuisha Halmashauri za Tandahimba, Kondoa Mjini, Kondoa Vijijini, Kilwa, Chalinze, Kigoma Mjini na Nyamagana. Amesema kanuni zinazuia mgombea kujiondoa kabla ya uteuzi.
"Taarifa tunazozikusanya zinaonesha kuwa upo mpango wa wasimamizi wa uchaguzi kuzichafua au kuziongea taarifa fomu za kugombea, ili kuwapotezea sifa za kuteuliwa wagombea wa ACT Wazalendo na vyama vingine vya upinzani," amedai Mwita.
Amemtaka Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, kusimamia kanuni na taratibu za uchaguzi huo, ikiwamo vyama kuchagua ngazi ya kudhamini wagombea wake.
Amesema chama hicho kimejiandaa kushiriki uchaguzi na kimesimamisha wagombea wa kutosha waliowapa mafunzo ya namna ya kujaza fomu vizuri.
Naye Msimamizi wa Uchaguzi Jiji la Dodoma, Dk. Fredrick Sagamiko, amekanusha shutuma zinazoenezwa katika mitandao ya kijamii kuwa zipo njama za kuwaengua baadhi ya wagombea wa vyama vya upinzani katika uchaguzi huo.
Ameyasema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini kuhusu shutuma hizo na mwenendo wa mchakato wa uchaguzi huo, akisisitiza hakuna taarifa yoyote ambayo imetolewa kuwa ni kiongozi wa chama gani ambaye amekosa sifa aliye na sifa ya kugombea katika uchaguzi huo.
Amesisitiza mchakato wa uchaguzi huo ni wa wazi, hivyo hakuna mkakati au nia yoyoye ya kuminya demokrasia kwa baadhi ya vyama vya siasa.
*Imeandaliwa na Restuta James na Elizabeth Zaya (DAR) na Paul Mabeja (DODOMA)
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED