Biteko: Bwawa la umeme Julius Nyerere liko salama

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:58 AM Apr 19 2024
Bwala la Umeme la Julius Nyerere (JNHPP).
PICHA: MAKTABA
Bwala la Umeme la Julius Nyerere (JNHPP).

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, amesema licha ya mvua zinazoendelea kunyesha nchini, Bwala la Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) lipo salama kutokana na kujengwa kisayansi na kuendelea kuzalisha umeme kupitia mtambo namba tisa huku mitambo mingine miwili ikiwa ukingoni kukamilika.

Alisema jijini Dodoma katika mahojiano kuhusu Maonesho ya Wiki ya Nishati 2024, yanayoendelea katika viwanja vya Bunge.

“Bwawa letu lipo salama kwani limejengwa kisayansi, ujazo wake wa maji ni mita za ujazo 183 na kwa takwimu za leo (jana) ni mita za ujazo 183.4, huko nyuma maji yalikuwa yakiingia mengi sana kwa kiasi cha mita za ujazo 8,400 kwa sekunde hivyo yalipaswa kupunguzwa ili kuendana na ujazo wa bwawa,” amesema Dk. Biteko.

Amesema, bila ya kuwapo kwa bwawa hilo athari za mvua zingeanza kuonekana tangu mwezi Oktoba, mwaka jana, lakini hali hiyo haikutokea mapema kwa sababu maji yalikuwa yakiijazwa katika bwawa kwa ajili ya kuzalisha umeme.

Aidha, Wizara ya Nishati na TANESCO ilishabaini uongezekaji wa maji katika Mto Rufiji, kuanzia mwezi Februari, mwaka huu na tahadhari ilianza kutolewa kuhusu kasi hiyo ya maji ili kuanza kuchukua hatua stahiki.

Dk. Biteko ameeleza kusikitishwa na athari zilizotokea kutokana na mafuriko ambayo yamesababisha maisha ya watu na mali zao na kuwa serikali inafanya kila jitihada kurejesha hali ya kawaida kwa wananchi waliokumbwa na maafa hayo.

Kuhusu utekelezaji wa ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia nchini, Dk. Biteko amesema, watu wengi bado wanatumia nishati isiyo safi ya kupikia kama mkaa na kuni na wananchi wachache wanatumia gesi na umeme.

Amesema lengo la serikali ni kuhakikisha kuwa ndani ya miaka 10, asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia na serikali imepitisha Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia ikiwa ni moja ya njia za utekelezaji wa ajenda hiyo ambayo inanadiwa na Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika kutekeleza mpango huo wa Nishati Safi ya Kupikia, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, imeshatoa waraka wa kutotumia kuni na mkaa kwa taasisi zinazozalisha watu kuanzia 100 na zaidi zikiwamo shule na Magereza.

Kuhusu upatikanaji wa umeme wa uhakika, Dk. Biteko amesema kwa sasa uzalishaji umezidi mahitaji na kinachofanyika sasa ni kuboresha miundombinu ya umeme ikiwamo ya kusafirisha umeme kwa kuwa baadhi ya sehemu, laini za umeme ni ndefu na kwamba vitajengwa vituo vya kupoza umeme takriban 83 nchini ili kuondoa athari za watu wengi kutopata umeme zitakapopata hitilafu.

Kuhusu bei ya gesi amekiri kuwa ni kubwa na kusema, serikali inaangalia kwa karibu suala hilo ili kupunguza gharama na hii haiishii kwenye gesi pekee bali kwenye majiko banifu na katika mwaka huu wa fedha serikali itaanza kutengeneza majiko ya bayogesi kwenye nyumba za wananchi wanaofuga mifugo ili watumie  nishati hiyo kwa ajili ya kupikia.