Biteko amsimamisha kigogo kampuni ya umeme

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:21 AM Mar 28 2024
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Dotto Biteko.
PICHA: HABARI LEO
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Dotto Biteko.

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Dotto Biteko, amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Fulcheshmi Mramba, kumsimamisha kazi Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ujenzi wa Miundombinu, Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO), Mhandisi Mohamed Abdallah, kwa kushindwa kusimamia vyema majukumu yake.

Dk. Biteko ametoa agizo hilo jana baada ya kufanya ukaguzi wa mradi wa kituo cha kupoza umeme cha Uhuru na kuonyesha kutokuridhishwa na utekelezaji wake kutokana na laini ya umeme kutoka Tabora hadi Urambo (kilometa 115) kuwa asilimia 10 tu. 

ETDCO ambayo ni kampuni tanzu ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) inasimamia utekelezaji huku ujenzi wa kituo cha kupoza umeme unaofanywa na kampuni ya TBEA kutoka China imetekeleza kwa asilimia 84.

Kutokana na kusuasua kwa ujenzi wa laini hiyo, Dk. Biteko ameagiza Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO kumwondoa Mhandisi Abdallah ambaye ameonekana kutotoa kipaumbele katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayosimamiwa na kampuni hiyo.

“Septemba 17, 2023 nilimtuma Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, kukagua mradi huu ambaye aliwapa maelekezo ya kukamilisha. Pia nilimtuma aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO, Meja Jenerali Paul  Simuli, kuja kukagua mradi huu Desemba 17, 2023. Naye  alitoa maelekezo ambayo hayajatekelezwa.

“Hatari iliyopo hapa ni kuwa TBEA atakamilisha kazi mapema Juni lakini umeme bado hautapatikana kwenye kituo kwa sababu laini ya umeme itakuwa haijakamilika,” amesema Dk. Biteko. 

Naibu Waziri Mkuu ameongeza kuwa kutokukamilika kwa wakati kwa laini ya umeme kutoka Tabora hadi Urambo, kutasababisha serikali kuilipa TBEA gharama za kuwapo eneo la mradi bila kazi ambayo ni asilimia 0.2 ya gharama za mradi, hivyo kuisababishia hasara serikali.

Amesema  TBEA na ETDCO zote zililipwa malipo ya awali ya utekelezaji wa kazi kwa asilimia 50 lakini ETDCO inatekeleza kazi kwa kusuasua huku TBEA ikifanya kazi kwa wakati.

Biteko amesema meneja mkuu huyo ameendelea kufanya kazi kwa mazoea na kusababisha kuchelewa kwa usambazaji wa nguzo na mpaka sasa zimepelekwa nguzo za umeme katika mradi wa ujenzi wa kituo hicho kwa asilimia 10 pekee wakati kazi imefikia asilimia 84 tofauti na matarajio.

“Hata hapa amemtuma mwakilishi huyo ni ‘size’ yangu. Katibu Mkuu tafuteni meneja mwingine huyo hafai. Sitataka  mazoea na mtu wala kampuni yoyote na lazima tuheshimiane katika kazi. Kuna udhaifu  mkubwa mwingi tu  tu nimeyasikia, uswahili mwingi na wizi ndani yake,” amesema.

Ujenzi  wa kituo hicho utakaogharimu Sh. Sh.bilioni 40  hadi kukamilika, utawezesha maeneo mengine kupata huduma ya umeme na kwamba vituo vingine vimejengwa  Sikonge eneo la Ipole kimefikia asilimia 89, Mlele aslimia 87 na Mpanda mkoani Katavi asilima 90 ikiwa  mistari asilima 47 imekwishajengwa na ni kilometa 393 kutoka Tabora.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO,  Mhandisi Athanas Nangali, amesema mradi wa ujenzi wa kituo hicho una msukumo wa umeme wa kilovati 132 kutoka Shinyanga hadi Tabora.

Aidha, Dk. Biteko ameitaka kampuni ya ETDCO kujitathmini katika utekelezaji wa miradi yake kutokana na miradi mingi kusuasua pamoja na kutathmini utendaji wake wa kazi ndani ya menejimenti ambao si wa kuridhisha.

Naye Mhandisi Sosipeter Mlalo wa shirika hilo, amesema kituo hicho kitapokea KV 132 na kitakuwa na transfoma yenye uwezo wa MW 35 na kwa sasa wilaya hiyo inatumia megawati saba. 

Mhandisi Mlalo amesema kutakuwa na njia tatu za kwenda Urambo,tatu za kwenda wialayani Kaliua ambapo katika kituo cha Urambo- Ipole wilayani Sikonge, ujenzi umefikia asilimia 88 ambapo Mkandarasi kutoka china TBEA anaendelea kufanya kazi nzuri.