‎Mkazi wa Tandika jijini Dar es Salaam, Daud Mahewa Chacha, ameiomba Serikali kuingilia kati mgogoro wa nyumba ya wazazi wake inayodaiwa kuuzwa na Benki ya CRDB kinyume na makubaliano ya mkopo, huku shauri hilo likiwa tayari lipo Mahakama Kuu, Kitengo cha Ardhi.
‎Akizungumza na waandishi wa habari akiwa na mama yake, Mgesi Maho, Daud amesema alikopa shilingi milioni 28 mwezi Mei 2021 kwa mkataba wa miaka miwili uliotarajiwa kuisha Mei 2023, akitumia nyumba ya wazazi wake iliyopo Tandika, Mtaa wa Kaburi Moja, kama dhamana. Ameeleza kuwa licha ya kukwama kwa muda kulipa marejesho kutokana na changamoto za kibiashara, benki iliwaita wadhamini na kikao kikafanyika Julai 22, 2022, ambapo walipewa siku 10 kulipa malimbikizo ili kusitisha mnada wa nyumba hiyo.
‎Daud amesema malimbikizo ya shilingi milioni 4.6 yalilipwa Julai 29, 2022 ndani ya muda uliokubaliwa, na baadaye mdhamini alikamilisha malipo yote ya mkopo hadi Februari 2023, kabla ya mkataba kuisha rasmi. Hata hivyo, anadai kuwa licha ya mkopo kulipwa kikamilifu, mchakato wa mnada uliendelea na nyumba kuuzwa Agosti 2, 2022 bila taarifa kwa familia, bila ushiriki wa viongozi wa Serikali ya Mtaa na kinyume cha taratibu za kisheria.
‎Kutokana na hatua hiyo, familia imefungua shauri Mahakama Kuu, Kitengo cha Ardhi, linalosikilizwa na majaji watatu. Daud ameongeza kuwa walipokea barua ya Mkuu wa Wilaya ya kuwataka wahame, barua wanayopinga uhalali wake wakisisitiza kuwa ni mahakama pekee yenye mamlaka ya kutoa maelekezo hayo wakati kesi ikiendelea.
‎Kwa upande wake, uongozi wa benki umeeleza kuwa mteja mwenye malalamiko anatakiwa kuwasilisha hoja zake kupitia Kitengo cha Malalamiko cha benki au Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa hatua zaidi.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED