Lloyd Austin adai Wapalestina lazima walindwe Gaza

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:47 AM Mar 27 2024
Waziri Austin amesema kuwa Israel lazima iwalinde Wapalestina katika mashambulizi yake huko Gaza.
PICHA: Anna Moneymaker
Waziri Austin amesema kuwa Israel lazima iwalinde Wapalestina katika mashambulizi yake huko Gaza.

WAZIRI wa Ulinzi wa Marekani, Lloyd Austin amesema ni jambo la kimaadili na kimkakati kuwalinda raia wa Kipalestina katika vita kati ya Israel na Hamas.

Austin ameyasema hayo katika mkutano na Waziri wa Ulinzi wa Israel, Yoav Gallant katika makao makuu ya ulinzi Pentagon wakati mahusiano kati ya Rais wa Marekani Joe Biden na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu yakizorota.

Waziri wa Ulinzi wa Israel pia alikutana na mshauri wa usalama wa taifa, Jake Suillivan, ambaye alimwambia Gallant kuwa Israel inahitaji kuongeza mmiminiko wa msaada wa kiutu huko Gaza.

Gallant baadae akafanya mkutano na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Upelelezi la Marekani - CIA William Burns aliyerejea kutoka kwenye mazungumzo ya Qatar yanayotafuta muafaka ambao haujapatikana bado wa Hamas kuwaachia zaidi ya mateka 130 wanaoendelea kushikiliwa Gaza.

Akizungumza na waandishi wa habari, Gallant, aliyeonekana kuituliza mivutano kati ya Marekani na Israel, alisema alisisitiza umuhimu wa mahusiano ya Marekani na usalama wa nchi yake na wa kulifanya jeshi la Israel kuwa bora zaidi katika kanda hiyo, ikiwemo mifumo yake ya angani.

Biden amejikuta chini ya shinikizo kutoka kwa makundi ya haki za binaadamu na baadhi ya Wademocratic wenzake wanaomtaka kuweka masharti kabla ya kutolewa msaada zaidi wa kijeshi kwa Israel.

DW