Israel yaishambulia vikali Gaza, 66 wauawa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:30 PM Mar 27 2024
Mtazamo kutoka eneo lililoharibiwa baada ya shambulio la Israeli huko Deir al-Balah, Gaza mnamo Machi 20, 2024. Israel inaendeleza mashambulizi makubwa katika eneo la Ukanda wa Gaza.
Ashraf Amra/Anadolu/picture alliance
Mtazamo kutoka eneo lililoharibiwa baada ya shambulio la Israeli huko Deir al-Balah, Gaza mnamo Machi 20, 2024. Israel inaendeleza mashambulizi makubwa katika eneo la Ukanda wa Gaza.

Israel imefanya mashambulizi makali katika eneo la Kusini mwa Ukanda wa Gaza licha ya shinikizo za kimataifa la kusitishwa mara moja kwa mapigano katika eneo hilo la Palestina linalokabiliwa na tishio la njaa.

DW imeripoti kuwa, Wizara ya Afya inayosimamiwa na kundi la wanamgambo wa Hamas katika eneo hilo, imesema mapema leo kwamba watu 66 wameuawa katika shambulizi hilo ikiwa ni pamoja na watu wengine watatu waliouawa katika shambulizi la Israel katika eneo la Rafah.

Mapigano hayo yameendelea siku mbili baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitisha azimio lake la kwanza la kutaka kusitishwa mara moja kwa mapigano na kutaka kuachiliwa kwa takriban mateka 130 ambao Israel inasema wamesalia Gaza, wakiwemo mateka 34 wanaodhaniwa kuwa wamekufa.

Wizara hiyo pia imesema, vikosi vya Israel vimezingira hospitali mbili katika eneo la Khan Yunis ambapo watu 12 wanaowajumuisha watoto waliuawa katika shambulizi la vikosi hivyo dhidi ya kambi moja ya wakimbizi.