WAKALA wa Vipimo (WMA) umelikabidhi Jeshi la Polisi katika Mkoa wa Kipolisi Ilala, Dar es Salaam, vifaa vya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) ikiwa sehemu ya kulisaidia kupambana na uhalifu wa aina mbalimbali ikiwamo udanganyifu katika mizani na vipimo.
Akikabidhi vifaa hivyo jana katika makao makuu ya polisi, Dar es salaam kwa niaba wa mtendaji Mkuu wa WMA, Meneja wa Vipimo Mkoa wa Ilala, Muhono Nashon, alisema msaada huo ni kutokana na ushirikiano wa muda mrefu katika masuala ya kazi baina ya WMA na Jeshi la Polisi hususani katika masuala ya jinai, ulinzi na usalama kwa maeneo mbalimbali ya ukaguzi.
Muhono alibainisha kuwa ushirikiano huo baina ya WMA na Polisi umekuwa na tija kutokana na jeshi hilo kudumisha hali ya amani na usalama kwa watumishi wa WMA na wananchi kwa ujumla katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo.
Pia alisema WMA imekabidhi vifaa hivyo ili kuunga mkono matumizi ya TEHAMA kwa taasisi mbalimbali za serikali likiwamo Jeshi la Polisi.
“Vifaa hivi vitatumiwa na Jeshi letu katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali na ni matumaini yetu kuwa vitaongeza ufanisi katika utendaji wake,” alisema Nashon.
Kamishna Msaidizi wa Polisi na
Ofisa Mnadhimu wa Mkoa wa Kipolisi Ilala, Kamishna msaidizi (ACP) Mohammed Makusi, aliishukuru WMA kwa msaada huo na kusisitiza kuwa jeshi hilo litaendelea kutumia TEHAMA katika utekelezaji wa majukumu yake ili kuwahudumia wananchi kwa ufanisi zaidi.
“Vifaa hivi vimekuja wakati muafaka tukielekea katika Wiki ya Maadhimisho ya Miaka 60 ya Jeshi la Polisi Tanzania ambayo yatafikia kilele chake Septemba 27, 2024,” alisema.
ACP Makusi alisema kaulinbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu ni ‘Huduma Bora za Kipolisi zitapatikana kwa Kubadili fikra, usimamizi wa sheria na matumizi ya TEHAMA’.
“WMA mmetuunga mkono katika TEHAMA, hivyo tunawashukuru kwa hiki mlichotupatia ambacho kitasaidia kuboresha huduma zetu,” alisisitiza Makusi.
WMA imekuwa na utaratibu endelevu wa kuimarisha ushirikiano na wadau na taasisi mbalimbali za serikali na binafsi kwa kutoa elimu ya matumizi sahihi ya vipimo, ushauri wa kitaalamu, semina elekezi na uwezeshaji kwa baadhi ya taasisi.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED