Wizara na ZEEA kuinua wanawake wajasiriamali Z’bar

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 07:13 AM Sep 07 2024
Waziri wa Wizara hiyo, Riziki Pembe Juma.
Picha: Mtandao
Waziri wa Wizara hiyo, Riziki Pembe Juma.

WIZARA ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto imeahidi kuendelea kushirikiana na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (ZEEA) katika kuwapatia wananchi fursa zitakazowasaidia kujikwamua kimaisha.

Fursa hizo pia zinalenga kuwajengea uwezo wananchi jambo ambalo ni chachu ya maendeleo yaliyokusudiwa na serikali.

Waziri wa Wizara hiyo, Riziki Pembe Juma, alisema hayo jana akiwa kwenye ziara katika Chuo cha Wajasirimali Wanawake cha Bare Foot Collage kilichoko  Kinyasini Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Alisema lengo la ziara yake ni kujifunza na kuona jitihada zinazofanywa na wanawake katika jamii, hivyo wizara itaendelea kushirikiana na ZEEA katika kuwapatia wanawake fursa na kuondokana na ugumu wa maisha.

Waziri Riziki alisema kila mwanamke ni kiongozi katika familia, hivyo serikali itaendelea kuwaunga mkono wanawake na kuwashauri wajasirimali wanawake kutovujinka moyo na kuzikabili changamoto wanazokutana nazo katika shughuli zao na kusisitiza kwamba hakuna mafanikio yasiyo na changamoto.

Aidha, Riziki aliwataka wanaume kuwaruhusu wake zako kwenda kujifunza  ujasiriamali na kubainisha kwamba kumekuwa na malalamiko kwa baadhi ya wanawake kutokupewa ruhusa na waume zao. Alisema hali hiyo inawarudisha nyuma wanawake kuleta maendeleo katika jamii.

Naye Mkurugenzi wa Bare Foot Collage, Brenda Ndossi, alisema  taasisi hiyo itaendelea kutoa elimu kwa wanawake ambao hawana ujuzi wowote ili kuwa na uwezo wa kusaidia jamii.

Mwezeshaji katika kituo hicho, Miza Juma Othman, aliishukuru serikali kwa kuwaka  mazingira mazuri ya kuwakomboa wanawake kimaisha, na kuiomba serikali kuendelea kuwaunga mkono wanawake hao waweze kufanya kazi kwa ufanisi.

 Mmoja wa wanafunzi waliopatiwa ujuzi, Fatma Haji Machano, kutoka  Shehia ya Zingwezingwe, aliwataka wanawake wengine ambao hawana kazi wala ujuzi kujiunga na kituo hicho ili kuondokana na umaskini.

Bare Foot College ina wanafunzi 21 wakiwamo 12 kutoka Zanzibar na tisa kutoka Somalia wanaojifunza utengenezaji wa taa za kutumia umeme wa jua.

Chuo hicho pia kinatoa ujuzi wa fani tofauti zikiwamo ufugaji nyuki, ushoni na elimu ya kilimo na tayari kimeshatoa wanafunzi 1,054 katika fani tofauti.