Wakulima wa mwani kutoka Kijiji cha Kikungwi, Mkoa wa Kusini Unguja, wamesema athari za mabadiliko ya tabianchi zimeendelea kuathiri kilimo chao.
Wamesema hali hiyo inasababisha zao hilo kuharibika kutokana na jua kali na mabadiliko ya kina cha maji ya bahari.
Wameeleza hayo leo Januari 26 wakati wakizungumza na Nipashe baada ya kupatiwa elimu kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi.
Pamoja na mambo mengineyo wamesema hali hiyo imepunguza kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa mwani na kuwakosesha matumaini ya kuendelea na kilimo hicho.
Mmoja wa wakulima hao, Bahati Issa, amesema kutokana na mabadiliko hayo, mwani unashindwa kustawi vizuri, hali inayowakatisha tamaa wakulima wengi.
Amesema kuwa suluhisho kubwa ni kulima mwani katika kina kirefu cha maji ya bahari, ili kukabiliana na jua kali, lakini wanakabiliwa na ukosefu wa vifaa.
Lipi Simai Suleiman, kutoka kijiji hicho, amesema wanahitaji ufumbuzi wa kutibu mwani ulioharibika kutokana na kukosa rutuba.
Pia, ameitaka serikali kuongeza bei ya mwani, akisema bei ya sasa ya kilo moja kununuliwa kwa Sh. 1,000 haikidhi mahitaji ikizingatiwa ugumu wa kilimo hicho.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Zaina Foundation Tanzania, Zaituni Njovu, amesema taasisi hiyo imeamua kutoa mafunzo kwa wajasiriamali na wakulima wa mwani, ili kuhamasisha mabadiliko chanya na matumizi ya teknolojia katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Amesema kilimo cha mwani kimeathiriwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo mabadiliko ya misimu yanayosababisha ongezeko la jua kali na kubadilika kwa kina cha maji ya bahari.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED