Wafanyabiashara walia kukithiri mikopo umiza

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:32 AM Oct 07 2024
Fedha
Picha: Mtandao
Fedha

WAFANYABIASHARA mkoani Mwanza wamesema kinachowakwamisha kuendelea kiuchumi, kukuza biashara zao ni kukithiri kwa mikopo yenye riba kubwa ‘mikopo umiza’.

Wamesema mikopo hiyo huwafanya kushindwa kutekeleza vyema kazi zao hali inayowafanya wengi wao kufilisika na kuwa maskini.

Walisema hayo juzi wakati wakizungumza na viongozi na maofisa wa benki ya Ecobank waliofika jijini hapa kutoa mafunzo ya kuendesha biashara, kukuza mitaji kwa wanawake na wafanyabiashara.

Mmoja wa wafanyabiashara hao, Lemison Owiso alisema ukubwa wa riba katika mikopo wanayokopa kupitia benki mbalimbali au kampuni zinazojihusisha na utoaji wa mikopo inasababisha wengi wao kufilisika.

Mkuu wa kitengo cha biashara wa benki hiyo, Joyce Ndyetabura alisema: "Wanawake wamekuwa wakiogopa kufanya biashara kubwa kwa sababu ya kukosa mitaji, wanaogopa kwenda kwenye benki kwa sababu hawana cha kuweka kama dhamana, sisi tunatoa mtaji kwa mwanamke yeyote ambaye anamradi uliyoanza kazi au tenda kwenye kampuni yoyote iwe binafsi au ya kiserikali, kikubwa iwe imesajiliwa kisheria.”