Vijana watakiwa kuacha kusubiri ajira serikalini

By Peter Mkwavila , Nipashe
Published at 11:05 AM Oct 28 2024
Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Kilimo, Mohamed Chikawe Chikawe (wapili kushoto) akiwa na vijana katika shamba la mfano.
Picha:Mtandao
Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Kilimo, Mohamed Chikawe Chikawe (wapili kushoto) akiwa na vijana katika shamba la mfano.

VIJANA nchini wametakiwa kuchangamkia fursa za kilimo, ili kujipatia kipato badala ya kusubiri ajira kutoka serikalini.

Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Kilimo, Mohamed Chikawe Chikawe, alitoa wito huo jana jijini hapa, wakati akizindua uanzishwaji wa kituo cha mafunzo ya kilimo na biashara kilichofadhiliwa na mashirika yasiyo ya kiserikali ya We- Effect, Oung World Feeders na Tanzania Youth Coalition.

Chikawe, alisema kilimo ni miongoni mwa sekta ambazo zina fursa nyingi za kuwasaidia vijana kujiajiri na kuajiriwa, badala ya kukaa kusubiri ajira serikalini.

"Serikali itaendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na vijana wanaojishughulisha katika sekta ya kilimo, kwa kuwa ni sehemu inayowapa ajira, niwaase wachangamkie fursa za taasisi na mashirika haya yasiyo ya kiserikali yanayojishughulisha na sekta ya kilimo, ili kujiimarisha kwenye uchumi badala ya kusubiri ajira," alisema.

Alisema serikali itaendelea kushirikiana na vijana ambao wanajikita katika sekta hiyo, kwa kuwapatia mafunzo na vifaa, kwa ajili ya kuwawezesha kujiinua kichumi zaidi.

"Taasisi kama hizi zimekuwa zikitoa mafunzo kwa vijana kuhusu kilimo, ndiyo maana serikali imekuwa ikishirikiana, kwa kuwa imekuwa msaada katika kuisaidia serikali kuajiri," alisema Chikawe.

Mkurugenzi wa Tanzania Youth Coalition, Lenin Kazoba, alisema mashirika hayo yamekuwa yakifanya kazi kwa malengo kuwasaidia vijana ushauri juu ya kukuza kipato na kuwaunganisha na masoko.

"Mradi huu unalenga kuwafikia vijana zaidi ya 11,606 wakiwamo wanawake 6,606 na wanaume 5,000 ambao kwa kuanzisha kituo hiki vijana watapewa mafunzo ya nadharia za kilimo biashara na uongozaji wa thamani," alisema.

Kazoba, alisema kuwa We- Effect itawanufaisha vijana kwa kuwapatia mafunzo ya mbinu za kilimo endelevu, usimamizi wa biashara utunzaji wa mazao, baada ya mavuno, upatikanaji wa fedha matuminzi ya teknojia na uhifadhi wa mazingira ya kilimo yanayozingatia mabadiliko ya tabia nchi.