WAFANYABIASHARA wa Halmashauri ya Mji wa Njombe mkoani Njombe, wameonywa kutumia dawa pasipo vipimo.
Pia, wameonywa matumizi ya dawa za binadamu kuwapa mifugo.
Onyo hilo lilitolewa mwishoni mwa wiki na Ofisa Elimu kwa Umma kutoka Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Maria Sanga, wakati akizungumza na wafanyabiashara wa soko kuu na soko la wakulima mjini humo.
Maria alisema wafanyabiashara hao wanatakiwa kuhakikisha wanatumia dawa kwa usahihi kama ambavyo wamepewa maelekezo na wataalamu kwa sababu bila ya kufanya hivyo kunapelekea usugu.
“Kumekuwapo na wimbi la wananchi kutumia dawa pasipo vipimo vya daktari, kutomaliza dawa kwa muda sahihi na wengine kutumia dawa za binadamu kwenye mifugo, niwaombe mkipata changamoto yoyote ya afya na daktari akakwambia tumia dawa hizi kwa muda wa siku kadhaa tumia muda huo huo,” alisema Maria.
Maria pia aliwataka vijana na wasichana ambao wamekuwa wakitumia dawa za nguvu za kiume na dawa za kuua mbegu za kiume maarufu (P2) zisitumike kila siku kwa sababu zinaharibu afya zao.
“Watu wamekuwa wakitumia P2 kila wakifanya tendo la ndoa, lakini kitaalamu inatakiwa zitumike mara mbili kwa mwaka na siyo kila wakimaliza tendo la ndoa,” alisema.
Aliongeza kuwa: “Kwa wanaume dawa za nguvu za kiume zipo kwa wale ambao wanachangamoto za maumbile yao ya mfumo wa uzazi na siyo kwa watu mbao wazima, mnajiua wenyewe vijana acheni kuwakomoa mabinti mkiamini dawa za nguvu za kiume zinawaridhisha wanawake, hapana.”
Naye Mkaguzi wa dawa kutoka TMDA Kanda ya Nyada za Juu Kusini, Adam Sorota aliwataka wananchi ambao watakutana na matatizo yoyote watoe taarifa katika kituo husika walichopata dawa.
Baadhi ya wafanyabiashara mjini Njombe, akiwamo Steward Muhiche alisema ili kuepuka usugu wa dawa elimu inapaswa kutolewa kwa jamii kwa sababu watu wengi bado wanatumia dawa kiholela bila ya kuwaona wataalamu wa afya.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED