Serikali kuongeza elimu ukuzaji viumbe maji

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 11:31 AM Sep 05 2024
Mkurugenzi wa Kuendeleza Ukuzaji Viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Nazael Madalla.
Picha;Mtandao
Mkurugenzi wa Kuendeleza Ukuzaji Viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Nazael Madalla.

SERIKALI imesema inalenga kuongeza elimu ya ukuzaji viumbe maji, ukiwamo uzalishaji vifaranga vya samaki hasa kaa ili kuongeza tija, mnyororo wa thamani na kupata soko la kimataifa.

Mkurugenzi wa Kuendeleza Ukuzaji Viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Nazael Madalla, amesema wamechukua hatua hiyo baada ya takwimu kuonesha dunia imekwishapoteza uvuvi wa asili.

Madalla aliyasema hayo juzi wakati wa mafunzo ya siku tano kwa wanazuoni vijana takribani 40 kwenye sekta ya uvuvi, kuwapa mbinu za ukuzaji viumbe maji, vikiwamo vifaranga vya samaki, yaliyofanyika katika Chuo cha Uvuvi Mbegani (FETA), wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani.

"Soko la baadhi ya viumbe maji kama kambale na kaa bado ni changamoto. Samaki aina ya kambale kuna baadhi ya imani za kidini kwamba hawali samaki asiye na magamba, pia kaa soko lipo ila hatua za vitotoreshi ni duni.

"Serikali imedhamiria kujenga vituo viwili vya uzalishaji vifaranga. Duniani imebainika kuwa mwaka 2022 katika takwimu asilimia 51 ya samaki walioliwa duniani, walitoka katika mazingira ya kufuga. Tanzania pia tunajitahidi kufikia asilimia 10 ya mazao yote uvuvi yanatokana na mazingira ya kufuga," alisema Dk. Madalla.

Mratibu wa mafunzo hayo, Lucka Mgwena, alisema lengo ni kuwajengea uwezo vijana wahitimu katika fani za sayansi ya viumbe maji (aquaculture) ngazi ya cheti, diploma na shahada ili wabaini fursa zilizopo kwenye ukuzaji viumbe hao nchini na kujiajiri.

"Vilevile, tunataka wawe na maarifa ya vitendo kwenye uzalishaji bidhaa, usimamizi na utafutaji masoko ya bidhaa zitokanazo na viumbe maji nchini. Maarifa yote yemejikita katika kuendeleza ukuzaji viumbe maji kibiashara," alisema Lucka.

Alisema kuwa, akiwa mmoja wa wanufaika na ufadhili wa masomo katika Shahada ya Uzamili wa Ukuzaji Viumbe Maji na Sayansi ya Uvuvi kupitia mradi huo, alifikiri namna ya kuwafikia vijana wahitimu ili kuwaongezea maarifa ya kuwawezesha kuzibaini fursa na kujiajiri.

Lucka alisema, mfadhili wa mafunzo hayo ni AQUAFISH – African Centre of Excellence in Aquaculture and Fisheries (ACE II) kupitia Chuo Kikuu cha Lilongwe cha Kilimo na Maliasili (LUANAR) cha Malawi.